Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Zanzibar
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameitaka Jumuiya ya Wazazi ya CCM kutumia rasilimali walizonazo katika kukijenga na kukieneza Chama cha Mapinduzi (CCM) katika maeneo mbalimbali ya nchi na kuzungumza na wananchi kuhusu kazi kubwa za maendeleo zinazofanywa chini ya Mwenyekiti wa chama hicho ambaye ni Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Biteko ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kundi la Wazazi, amesema hayo wakati akizungumza na Viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM-Zanzibar wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Dogo Mabrouk kikao kilifanyika katika Ofisi Kuu ya CCM iliyopo Kisiwandui, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Dkt. Biteko amesema kuwa Mwenyekiti wa Mkoa, Katibu wa Mkoa au kiongozi yoyote yule, kwa kutumia rasilimali alizonazo atembele maeneo ya Mkoa wake, Wilaya na Vijiji hata mara moja na kuzungumza na makundi mbalimbali ikiwemo Wajumbe wa Kamati za utekelezaji za Jumuiya yao na kuwaeleza kuhusu masuala ya kujenga na kueneza chama.
“Hii inawezekana, tujipange, tufanye ziara hata kama ni kidogo, polepole tutafanya makubwa kadri tutakavyoendelea, tuwe mstari wa mbele kueleza mafanikio ambayo CCM na Serikali yake wameyafanya,”amesisitiza Dkt. Biteko
Amesema kuwa, Jumuiya ya Wazazi ya CCM ni jumuiya kubwa ndani ya chama hivyo inapaswa kufanya kazi za kukijenga kwa ukubwa huo kwa kuwa inabeba makundi yote ndani ya CCM na haina mipaka au ukomo wa mtu kuwa sehemu ya jumuiya.
“Nikitolea mfano Jumuiya yetu ya Wanawake, inahusu wanawake katika chama, Jumuiya ya Vijana umri fulani ukifika unakuwa hauna vigezo, lakini Jumuiya hii haina mipaka hivyo inapaswa kuwa na nguvu kubwa, tutumie ukubwa wake ili kuwasaidia Mwenyekiti wetu na Makamu Mwenyekiti upande wa Zanzibar katika kujenga chama na kuzungumza kwa ukubwa yale yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika,”ameeleza Dkt. Biteko
Ameongeza kuwa, Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu Mwenyekiti wa CCM kwa upande wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi wanataka kuona viongozi wa chama katika ngazi mbalimbali wanawasaidia kazi ikiwemo ya kueleza mafanikio makubwa ya kimaendeleo yanayoendelea kufanyika na kazi kubwa inayofanywa na viongozi hao katika kuwaunganisha Watanzania, kuwa na maridhiano na kujenga uchumi wa nchi.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Dogo Mabrouk amemshukuru Dkt.Biteko kwa kuithamini jumuiya hiyo kwa kuiwezesha kwa vitendea kazi ambavyo vitaboresha utendaji kwenye mikoa sita ya Zanzibar na kuahidi kuwa wataendelea kumpa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kabla ya kufanyika kwa kikao hicho, Dkt. Biteko alizuru katika Kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume.
Dkt Biteko ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, amekabidhi pikipiki sita na kofia ngumu kwa ajili ya Jumuiya ya Wazazi (CCM), Zanzibar kwenye Mikoa sita ya kisiwani hicho.
Amesema kuwa, pikipiki hizo ni mali ya Jumuiya ya Wazazi (CCM) ambapo ameelekeza kuwa, pikipiki hizo zikafanye kazi ya siasa kama ilivyokusudiwa.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua