March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jumuiya ya Maridhiano kufanya maombi ya siku tatu kuliombea Taifa

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online-Dodoma

JUMUIYA ya Maridhiano na Amani Tanzania(JMAT),imetoa tamko la kuomba kufanyika maombi ya kitaifa yatakayotanguliwa na mfungo wa siku tatu ili kuliombea Taifa kutokana kadhia iliyotokea Octoba 29,2025,wakati wa uchaguzi mkuu nchini iliyosababisha hasara za watu kupoteza maisha, uharibifu wa mali za serikali na watu binafsi pamoja na uharibifu wa miundombinu.

Akitoa tamko la Jumuiya hiyo leo mbele ya waandishi wa habari Jijini Dodoma,Mwenyekiti wa JMAT,Sheikh Dkt.Alhad Mussa Salum,amesema kadhia hiyo imesababisha kuzaa chuki na athari ya kisaikolojia katika akili na mioyo ya watu na kuleta hisia za udini jambo ambalo linatakiwa kushughulikiwa mapema.

“Kufanyike maombi ya kitaifa yatakayotanguliwa na mfungo wa siku tatu,maombi yawe ya kina kws watu wa Imani na madhehebu mbalimbali,kumuomba Mungu msamaha na toba ya kweli na kumuomba Mungu roho ya kutoa msamaha tulipokosewa na wenzetu,

Maombi yaratibiwe na kufanyika kitaifa na pia kwa sababu JMAT ipo vizuri mikoani na wilayani,maombi pia yafanyike katika maeneo mbalimbali kwa mikoa yote na wilaya zote kwa namna moja na siku moja nchi nzima mwenyezi Mungu atatenda na kuliponya Taifa,”alisema.

Amesema maombi hayo yawe ya kina kwa watu wa imani na madhehebu mbalimbali na yaratibiwe na kufanyika kitaifa kwa namna moja na siku moja nchi nzima.

Pia ameomba yafanyike maridhiano ya kisiasa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukaa na viongozi wa vyama vya siasa pamoja na uwakilishi wa viongozi wa dini wanaoaminika katika kuwa na fikra njema,huru na misimamo thabiti ili kuunda mwanzo mpya wa kuimarisha mifumo ya kusaidia kuongoza nchi kwa kuaminiwa na wote.

Mbali na hayo wameiomba serikali kuchukua hatua za makusudi kubaini raia halali wa nchi hii na wageni wanaoingia ili kutambua nia na madhumuni yao.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa JMAT, Askofu Israel Maasa ameshauri matumizi ya mitandao kudhibitiwa kwa sababu ni njia kubwa iliyotumika kusambaza uharibifu na jambo kubwa linaloweza kujitokeza.

Naye, Chifu Mkuu wa Wamasai, Isack Meijo amesema watu wachache ndiyo wanarubuni vijana vijana kufanya vurugu wakiwemo wenye tamaa waliopo ndani na nje ya nchi hivyo ni vyema wadhibitiwe.

Pamoja na maombi hayo JMAT imempongeza kwa dhati na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Dkt.Samia Suluhu Hassan,na serikali yake kwa kulifungua kanisa la ufufuo na uzima na kusema hatua hiyo ni muhimu katika kuleta ustawi wa serikali na waumini wa dini mbalimbali.