Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Legal Services Facility (LSF) wamezindua Jukwaa la Kitaifa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi (National Women Economic Forum) ili kuwafikia wanawake katika sekta mbalimbali za uchumi na hatimaye kuliwezesha kundi hilo kufikia fursa zinazowazunguka.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Jukwaa hilo uliofanyika Jijini Dodoma mnamo 17 Mei 2023, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa, jukwaa hilo limeanzishwa ili kuongeza uelewa kwa wanawake kuhusu masuala ya Biashara, upatikanaji mitaji na Sheria za nchi katika masuala ya uchumi.
Aidha ameongeza kuwa serikali imeendelea kutekeleza mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa kuhusu kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi, na kubainisha kwamba mbali na jukwaa hilo la kitaifa, Serikali imeunda majukwaa ngazi ya mkoa katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.
“Kupitia maazimio ya mkutano wa wanawake Beijing 1995, Tanzania iliamua kujikita katika maeneo manne ambayo ni: kuwawezesha wanawake kiuchumi; wanawake na haki za kisheria; usawa katika elimu, mafunzo na ajira; na wanawake katika nafasi za uongozi na ngazi za Maamuzi.” amesema Dkt. Gwajima.
Vilevile Dkt Gwajima amewataka viongozi wa majukwaa kutoka mikoa mbalimbali kusimamia majukwaa haya kikamilifu kwa kuwaunganisha wanawake na fursa za kibenki, masoko, na kuboresha utaalamu katika uzalishaji wa bidhaa zao huku akiwapobgeza viongozi wa kitaifa na kuwasisitiza kuwa, wanalo jukumu kubwa katika kusimamami jukwaa hili ili kwenda sambamba na kasi ya Rais Dkt. Raisi Samia Suluhu ya kuwainua wanawake kiuchumi na kuondoa vitendo vya ukatili wa kijinsia
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala, amesema Shirika hilo imeamua kushirikiana na Serikali katika uzinduzi wa jukwaa hilo, kwa kuwa linagusa moja ya maeneo muhimu ya utekelezaji wa programu ya upatikanaji wa haki kwa watu wote hususani wanawake ili kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“Ni matumaini yetu kuwa Jukwaa hili la kitaifa litajikita katika kusghulikia changamoto mbalimbali za wanawake kwenye masuala ya kiuchumi, masuala ya kisera, kitaaluma, kirasilimali pamoja na haki nyingine za msingi za kiuchumi. Sisi kama LSF tutaendelea kushirikiana na Jukwaa hili kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii,” amesema Ng’wanakilala.
Uzinduzi wa Jukwaa hilo umeenda sambasamba na uteuzi wa viongozi wake wakiwemo Mwenyetiki Taifa, Fatuma Kange Makamu Mwenyekiti Taifa, Neema Ndossi Katibu Taifa, Dkt. Regina Malima Katibu Msaidizi Taifa, Neema Kajala pamoja na Mhasibu Taifa Angel Kessy.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja