December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Juhudi za Rais Samia zakuna nchi za Afrika

*Sasa mkutano mkuu wa Nishati Barani Afrika kufanyika Tanzania, nia ni kukusanya dola za Marekani bilioni 190/- za kusambaza umeme

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline

TANZANIA inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa masuala ya nishati barani Afrika utakaotafuta namna ya kukusanya dola za Marekani bilioni 190 ili zitumike kufikisha umeme kwa wananchi milioni 300 barani humo ifikapo mwaka 2030.

Hatua hiyo inatokana na mkakati wa Serikali ya awamu ya sita kupeleka umeme vijijini na vitongojini kwa kasi hali ambayo imezivutia taasisi za Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kuamua kufanya mkutano huo mkubwa ifikapo Januari, 2025.

“Wameridhishwa na utendaji kwenye sekta ya nishati, wameridhishwa na mkakati wa Serikali wa kupeleka umeme mpaka vijijini, siyo tu vijijini lakini mpaka kwenye kila nyumba.

Wameamua kuitisha mkutano mkubwa barani Afrika ambao utawakutanisha wadau mbalimbali, taasisi za Kimataifa na taasisi zinazotoa mikopo kwa wajasiriamali na makampuni ili waweze kuwekeza kwenye umeme.”

Hayo yalisemwa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye mkutano wa kujadili ajenda ya upatikanaji wa nishati Afrika ulioandaliwa na taasisi ya Global Energy Alliance for People and Planet (GEAPP) jijini New York, Marekani.

Akizungumza na washiriki wa mkutano huo uliofanyika kwenye ofisi za taasisi ya Rockefeller, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa baraka zake ili Tanzania iwe mwenyeji wa mkutano huo.

Alisema mkutano huo ambao utaendeshwa kwa pamoja baina ya Benki ya Dunia, Benki ya ADB na Kamisheni ya Umoja wa Afrika, unatarajiwa kuwaunganisha viongozi wa dunia, waatalamu wa kutoka viwandani, asasi za kiraia katika kutafuta namna ya kuwezesha upatikanaji wa nishati za uhakika, teknolojia bora za nishati safi na sera endelevu.

“Ninaipongeza Serikali ya Norway na taasisi ya Rockefeller kwa kuamua kuunga mkono jitihada za Benki ya Dunia na ADB za kuhakikisha umeme unapatikana kwa watu milioni 300 ifikapo mwaka 2030.

Mpango huu ni wa muhimu hasa kwa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara ambako watu zaidi ya milioni 600 hawana fursa ya kupata umeme.

Hatuwezi kuwa na maendeleo endelevu kama hatutashughulikia kwa haraka changamoto hii,” alisema.

Waziri Mkuu alizishukuru Benki ya Dunia na AfDB kwa ahadi yao kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali ili kufanikisha mkakati wa Tanzania wa kupeleka umeme kila nyumba uwe umekamilika ifikapo 2030.

Mapema, Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina alisema wanawake milioni 900 wanataabika kwa kukosa nishati safi ya kupikia na kila mwaka ilhali upishi unapaswa uwe ni wa staha.

“Wanawake milioni 130 wanatakiwa wawe wamefikiwa na huduma hii kila mwaka. “Tunapoteza wanawake na watoto wengi kwa sababu ya kukosa huduma hii.”

Dkt. Adesina alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia vema sekta ya nishati na hasa uzalishaji wa nishati safi ya kupikia na kwamba anataka kuona ifikapo mwaka 2030, malengo ya kuhama kutoka kupikia kuni na mkaa kwenda nishati safi yawe yametimia.

Wakati huohuo, Rais wa Liberia, Joseph Boakai ambaye pia alishiriki kikao hicho, alisema umeme ni suala la muhimu sana kwenye maisha ya mwanadamu na linapaswa kupewa kipaumbele kikubwa kwani bila umeme hakuna maendeleo.

Alisema nchini Liberia ni asilimia ndogo tu ya nchi hiyo ndiko wanapata umeme na tena kwenye maeneo ya mji mkuu. “Nchini Liberia, maeneo mengi ya vijijini yako gizani, na maeneo yenye umeme hayafikii asilimia 20.

Unawezaje kupanga ajenda za maendeleo kama hauna umeme? Unawezaje kwenda hospitali wakati hakuna umeme? Hili ni suala nyeti na hatupaswi kuendelea kulisubiria kwa muda mrefu,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Tanzania inaungana na mataifa mengine ambayo yanaunga mkono mkakati wa hatuna haja ya kumuacha mtu nyuma katika suala zima la ujenzi wa kesho iliyo bora kwa vijana.

Alitoa kauli hiyo wakati akichangia mada kwenye mjadala wa The Future Starts Now uliokuwa sehemu ya kuhitimisha Mkutano wa siku mbili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kujadili Hatma ya Siku Zijazo (Summit of the Future) ulioanza juzi kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani.

“Kuna haja ya kuwaandaa vijana wetu ili wawe watu bora. Tuanze nao leo, tusisubiri kesho. Tuwape fursa za kushiriki kwenye kilimo, mifugo, uvuvi na uchumi wa bluu kwa ujumla wake.”

Waziri Mkuu ambaye yuko Marekani akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan leo atashiriki ufunguzi rasmi wa Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA79).

Waziri Mkuu ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kitaifa, Balozi Thabit Kombo, Waziri wa Nchi (OR-Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo na Waziri wa Afya wa SMZ, Nassor Ahmed Mazrui na watendaji wengine wa Serikali.