October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JPM awashukuru waumini Parokia ya Bikira Maria

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Dodoma

RAIS John Magufuli amewashukuru waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Imakulata, Ikulu-Chamwino Mkoani Dodoma kwa kuanzisha harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti wa Chamwino ambao umekamilika na kuanza kutumika.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akishukuru baada ya kupokea Sakramenti Takatifu toka kwa Padre Paul Mapalala wakati wa Misa ya Dominika ya 32 Mwaka “A” katika Parokia ya Bikira Maria Imakulata Chamwino Ikulu Dodoma

Rais Magufuli aliyeongozana na mkewe Mama Janeth Magufuli ametoa shukrani hizojana jijini Dodoma katika Misa Takatifu ya Jumapili ya 32 ya Mwaka “A” iliyoongozwa na Paroko wa Parokia hiyo Padre Paul Mapalala.

Amewashukuru waumini wa madhehebu mengine ya Dini waliojitokeza kuchangia ujenzi wa Msikiti huo pamoja na Kanisa la Bikira Maria Imakulata Ikulu-Chamwino ambalo ujenzi wake ulifanyika kabla, na amebainisha kuwa kitendo hicho kinadhihirisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati walionao Watanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli akishiriki
ibada ya Misa ya Dominika ya 32 Mwaka “A” katika Parokia ya Bikira Maria Imakulata Chamwino Ikulu Dodoma

Aidha, Rais Magufuli ambaye jana amesali Ibada ya kwanza ya Jumapili tangu aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili amewashukuru Waumini wa Madhehebu yote ya dini kwa sala na dua zao za kuombea mchakato wa uchaguzi mkuu tangu wakati wa kampeni hadi kuapishwa kwake na amesisitiza kuwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais ni ushindi wa Watanzania wote.

Amewaomba viongozi wa dini na Watanzania wote kuendelea kuliombea Taifa, na kuiombea Serikali anayoiongoza ili itekeleze ahadi zilizomo katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020/25 zilizolenga kujenga uchumi imara na ustawi wa jamii.