Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
ALIYEKUWA Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe na Miss Tanzania nambari mbili 2006, Jokate Mwegelo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini kwa kumteua tena kuwa Mkuu wa Wilaya Temeke, Dar es Salaam.
Rais Samia, amemteua Jokate kuwa mkuu wa Wilaya ya Temeke akichukua nafasi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Godwin Gondwe ambaye kwa sasa ameamishiwa Wilaya ya Kinondoni.
Akitoa shukrani hizo kupitia kwenye Ukurasa wake wa Instagram Jokate amesema, anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kumpatia zawadi ya uhai ili kulitumikia vyema Taifa la Tanzania.
“Kwanza, kwa unyenyekevu mkubwa namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutupatia sote zawadi ya uhai. Pili, kwa namna ya kipekee, ninamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini na kunipa nafasi ya kumuwakilisha na kutoa mchango wangu wa kuwatumikia Watanzania wenzangu na WanaTemeke kupitia majukumu ya Ukuu wa Wilaya.
“Tatu, Shukrani zangu nyingi kwa Viongozi, Watendaji, na Wananchi wenzangu wa Wilaya ya Kisarawe. Kwa mashauri na ushirikiano mzuri kwa kipindi chote tulichokuwa tukihudumu pamoja, kupitia umoja na mshikamano wetu tulifanikisha mengi na kutatua baadhi ya changamoto zilizokuwa zinaikabili Wilaya ya Kisarawe.
“Nne, kwa upande wa Wananchi wenzangu wa Temeke, Viongozi na Watendaji wote, ninawasihi na kuwaomba ushirikiano wenu. Mimi ninawaahidi Utumishi wa pamoja na uliotukuka kwa manufaa ya Temeke yetu. Lengo letu kubwa liwe kuiona Temeke inayofanya vizuri zaidi kuanzia pale mlipopafikisha wezangu katika Sekta ya Elimu, Afya, Michezo, Biashara na Uwekezaji, Usafiri wa Umma, Sanaa, fursa za Ajira, usimamizi wa Miradi ya Maendeleo na Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali.
Mwisho, ninawashukuru sana Ndugu, Jamaa, Marafiki, na Wote kwa pongezi zenu na kunitakia kheri kwenye kituo changu kipya cha Utumishi. Ahsanteni tena,” amesema Jokate.
Katika hatua nyingine Bodi ya Filamu Tanzania imempongeza Jokate Mwegelo, Simon Simalenga na Juma Chikoka maarufu kama ‘Mchopanga’ kwa kuteuliwa kuwa wakuu wa Wilaya na kuwataka kutekeleza majukumu yao ipasavyo wakiwa kama wadau wa filamu hapa nchini.
More Stories
Mzee wa Bwax afunika ‘Kitaa food Fest’ Mbagala
TBL yazindua Kampeni ya ‘Smart Drinking’
Msimu wa nne,tuzo za eagle entertainment, kufanyika kivingine