November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JKT na mkakati wake wa kufufua zao la mkonge mkoani Tanga

Na Joyce Kasiki,Tanga


JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limelima ekari 107 za shamba la mkonge katika kikosi 835 KJ Mgambo kilichopo  mkoani Tanga ambapo kati ya hizo ekari saba ni kwa ajili ya kuzalisha mbegu bora ya zao hilo.
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi wa JKT  ambaye pia ni Katibu wa Kilimo Mkakati wa Jeshi hilo Kanali Peter Lushika wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ziara yake ya kukagua shamba hilo la mkonge ambalo limelimwa zao hilo kwa mara ya kwanza katika kikosi hicho.
Kanali Lushika amesema,kilimo hicho cha mkonge katika kikosi hicho ni utekelezaji wa agizo la Serikali la kuzitaka taasisi mbalimbali nchini kulima mazao ya kimkakati yenye lengo la kulikomboa Taifa kiuchumi.
Vile vile alisema,kilimo hicho ni utekelezaji wa Mpango wa kilimo mkakati ndani ya Jeshi hilo la kuhakikisha linajitegemea hasa katika kujilisha.
“Katika kikosi hiki pamoja na mazao mengine ya kimkakati ,mwaka huu tumeanzisha kilimo cha zao la mkakati ambapo tumelima ekari 107,katika ekari hizo,ekari 100 ni kwa ajili ya kuvunwa baada ya kukomaa na ekari saba ni kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu bora ya zao la mkonge.” Amesema Kanali Lushika na kuongeza kuwa
“Tumeamua kulima kitalu hicho  cha mbegu ili kupata mbegu bora zitakazotuwezesha kupata katani bora,lakini pia hii itatusaidia kupunguza gharama za kuagiza mbegu nje ya nchi.”
Aidha alisema,JKT pia limekuwa likilima mazao mbalimbali kupitia mpango wake wa kilimo mkakati ambapo limekuwa likilima mazao ya kimkakati ya Jeshi hilo lakini na mazao ya kimkakati yakiwemo ya mahindi,mpunga,michikichi,korosho,kahawa.
Anesema katika mpango huo wa kilimo mkakati pia wanajenga viwanda vya kuchakata mazao kwa lengo la kuyaongeza thamani lakini pia wanajenga maghala kwa ajili ya kuhifadhi mazao katika hali ya usalama.
“Katika eneo hilo tumedhamiria kuhakikisha Taifa linakuwa na usalama wa chakula ,maana Taifa haliwezi  kuwa na chakula bora bila kuwa na usalama wa chakula hicho.”
Kwa upande wake  Kaimu Kamanda Kikosi wa kikosi cha 835 JKT Mgambo Meja  Raymond Mwanri amesema kuwa walianza kutekeleza agizo la Seriki kwa kulima ekari 100 za Mkonge Juni mwaka huu.

“Baada ya maandalizi ya shamba hili tulianza kupanda mkonge septemba mwaka huu na tunatarajia kuvuna baada ya miaka mitatu.”
Naye kijana wa kujitolea katika kikosi hicho Hamad Hamisi Shame alisema ameishukuru Serikali kwa kuwapa fursa hiyo ya  kujengewa na kujifunza kwa vitendo shughuli mbalimbali za uzalishaji mali katika Kambi hiyo huku akisema ujuzi wanaoupata utawasaidia kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi pindi watakaporudi uraiani.