January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JKT Mbweni watetea ubingwa netiboli

Mathew Kwembe, Arusha

TIMU ya JKT Mbweni ya Dar es Salaam imefanikiwa kutetea ubingwa wake wa Netiboli Ligi Daraja la Kwanza mwaka huu baada ya kuwafunga Mabingwa wa Kombe la Muungano la Netiboli mwaka 2019 TAMISEMI Queens goli 40-39 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

TAMISEMI wakiongozwa na nahodha wa timu hiyo Sophia Komba na wafungaji wake hatari Lilian Jovin na Aziza Itonye waliutawala mchezo huo mwanzo hadi mwisho wa mchezo na kuwafunika kabisa wachezaji Frida Zablon na Doritha Mbunda wa JKT Mbweni ambao iliwabidi kutumia nguvu kuwakaba wachezaji wa TAMISEMI.

Hadi robo ya kwanza ya mchezo inamalizika TAMISEMI walikuwa mbele kwa magoli 10-8, robo ya pili na ya tatu TAMISEMI Queens waliongoza kwa magoli 19 -18 na robo ya tatu waliongoza kwa magoli 29-28.

Nyota wa mchezo huo alikuwa ni mchezaji Aziza Itonye (GA) wa TAMISEMI ambaye mara kwa mara alikuwa akiipasua ngome ya JKT Mbweni na kulazimika kufunga magoli akiwa mbali kwa kuhofia kufanyiwa faulo na wachezaji wa JKT.

Mchezo huo ambao ulishuhudiwa na Naibu Waziri Wizara ya Habari Utamaduni sanaa na Michezo Paulina Gekul ambaye aliwataka CHANETA kuhakikisha katika mashindano yajayo ihakikishe inateua waamuzi bora na wenye weledi wa kuchezesha mashindano ya ligi daraja la kwanza nchini baada ya waliochezesha fainali hiyo kushindwa kusimamia sheria ipasavyo.

Kauli ya Naibu Waziri iliungwa mkono na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Athumani Kihamia ambaye baada ya kumalizika kwa mchezo huo alionyesha dhahiri kukerwa na Kitendo cha mwamuzi kushindwa kuumudu mchezo huo.

“Kumeonekana kuwa mapungufu kwa kiasi kikubwa kwa upande wa waamuzi. Huyu refa aliyechezesha leo kutoka Mwanza mimi siwezi kumung’unya maneno hakuchezesha kihalali na tunaweza kusema ameyatia aibu mashindano haya,” amesema Dkt Kihamia.

Dkt. Kihamia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Michezo mkoa wa Arusha amesema, anatarajia tukio kama hilo hataliona mwakani katika mashindano ya Ligi daraja la kwanza na badala yake aliwataka CHANETA kuhakikisha kuwa mashindano hayo yanaamuliwa na marefa walio huru na uwezo.

“Kwa refa kuchezesha vile ama hana uwezo au kachukua rushwa ama timu mojawapo inamhusu, kwa hiyo mwakani tutahakikisha mambo ya namna hii hayatokei katika mkoa wetu,” amesema Dkt Kihamia.

Katika mashindano hayo Timu ya TAMISEMI ilifanikiwa kutoa mfungaji bora wa mashindano hayo Lilian Jovin, Mchezaji bora wa mashindano hayo (MVP) Meryciana Kizenga na Mchezaji bora wa kati wa mashindano hayo Sophia Komba.

Jumla ya timu 13 zilishiriki mashindano hayo yaliyoanza julai 19 na kuhusisha timu tisa za wanawake na timu nne za wanaume, ambapo washindi watatu wa kwanza wataiwakilisha nchi katika mashindano ya Netiboli Afrika Mashariki na timu sita za mwanzo zitashiriki katika kombe la Netiboli Zanzibar katika mashindano yatakayofanyika baadaye mwaka huu.