January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JKT laita vijana wa kujitolea,latahadharisha wananchi dhidi ya matapeli

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

JESHI lakujenga Taifa limetangaza nafasi za vijana wa kujitolea kwa mwaka 2024 huku likiwaasa wazazi na walezi kujihadhari na matapeli ambao wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kutapeli wananchi kwamba wanaweza kuwasaidia kupata nafasi hizo kwa kutoa fedha.

Akizungumza Makao Makuu ya JKT Chamwino mkoani Dodoma na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajab Mabele kuhusu wito wa vijana hao kwa mwaka 2024,Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala Kanali Juma Mrai amesema,mara nyingi nafasi hizo zinapotangazwa wanaibuka matapeli ambao hudai nafasi hizo zinapatikana kwa kutoa fedha.

“Ieleweke nafasi hizi ni bure haziuzwi,na nafasi hizi ni kwa ajili ya vijana wote wa kitanzania cha muhimu awe amekidhi vigezo vilivyoainishwa hivyo JKT halitahusika kwa namna yoyote ile pale mzazi atakapotapeliwa kwa kutoa fedha ili kupata nafasi hizo.”

Aidha amesema utaratibu wa kuomba na hatimaye kuchaguliwa kujiunga na mafunzo hayo unaratibiwa na ofisi za wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ambako mwombaji anaishi.

Kanali Mrai amesema Usajili wa vijana hao kujiunga na mafunzo ya JKT utaanza Oktoba Mosi mwaka huu kwa mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani ambapo vijana watakaochaguliwa watatakiwa kuripoti kwenye makambi ya JKT kuanzia Novemba Mosi hadi 3 mwaka huu.

Vile vile JKT limewataarifu vijana watakaopata fursa hiyo kuwa,JKT halitoi ajira ,pia halihusiki kuwatafutia ajira katika asasi ,vyombo vya ulinzi na usalama na mashirika mbalimbali ya Serikali na yasiyo ya kiserikali bali huta mafunzo ambayo yatawasaidia vijana kujiajiri wenyewe mara baada ya kumaliza mkataba wao na JKT.

“Sifa za mwombaji na maelekezo ya vifaa wanavyotakiwa kwenda navyo yatapatikana katika Tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz.”amesisitiza Kanali Mrai na kuongeza kuwa

“Mkuu wa JKT Meja Jenerali Mabele anawakaribisha vijana wote watakaopata fursa hiyo kuja kujiunga na vijana wenzao ili kujengewa uzalendo,umoja wa Kitaifa,ukakamavu,kufundishwa stadi za kazi,stadi za maisha na utayari wa kulijenga na kulitumikia Taifa lao.”