January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JKT yajidhatiti kukabiliana na uhaba wa mafuta ya kula nchini

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limesema limejipanga kuhakikisha linapunguza uhaba wa upatikanaji wa mafuta ya kupikia uliopo nchini kwa kuzalisha kwa wingi mazao ya mafuta lakini pia kwa kuzalisha mbegu bora za mazao hayo zitakazoleta uzalishaji wenye tija hapa nchini.

Akizungumza  wakati alipotembelea shamba la uzalishaji wa mbegu bora za alizeti  lenye ukubwa wa ekari 500 lililopo kijiji cha Chenene wilayani Chamwino katika mkoa wa Dodoma,   Mkuu wa Tawi la Utawala Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema,uzalishaji wa mazao ya mafuta kwa wingi na uzalishaji wa mbegu bora utachangia kwa kiasi kikubwa kumaliza changamoto hiyo hapa nchini.

“Uhitaji wa mafuta ya kupikia hapa nchini ni tani 650,000,lakini  upatikanaji wake ni tani 290,000  hivyo upungufu uliopo tani 360,000,kwa hiyo JKT tumejipanga kwa kushirikiana na Serikali kuhakiki tunaondoa upungufu huo.”amesema na kuongeza kuwa

“JKT tumejikita katika kilimo, Mifugo na Uvuvi ambapo kwa  upande wa chakula tumejitosheleza na sasa tunataka tujikite katika uzalishaji wa mazao ya mafuta ,na hapa tumeanza na uzalishaji wa mbegu ya zao la alizeti ili kuhakikisha mbegu bora inapatikana JKT na wakulima wapate mbegu bora”.

Aidha amesema,JKT  kwa kushirikiana na Taasisi ya utafiti wa kilimo TARI, kituo cha Ilonga walifanya utafiti wa udongo na kuthibitika kuwa na kiwango kinachotakiwa katika uzalishaji wa zao la alizeti na kuhakikisha mbegu inayozalishwa ni ya uhakika itakayomsaidia mkulima tofauti na mbegu nyingine zinazotumika msimu mmoja.

Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Mabena ,kuhusu zao la mchikichi katika kikosi 821 KJ Kigoma zimelimwa ekari 800 za mbegu za msingi wakati ekari 1200 zikiandaliwa lengo ni kufikia uzalishaji katika ekari 2000 zitakazozalisha mbegu za Mchikichi ambazo zitatumika katika Halmashauri zinazolima zao hilo.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kutoka JKT Kanali Peter Lushika amesema katika ekari 500 zilizolimwa katika eneo la Chenene  zitazalishwa tani 600 za mbegu za alizeti huku lengo ni kufikia tani 1300 hadi tani 1500 za mbegu bora ya zao hilo aina ya Records.

“Mbegu hizi tutazitawanya kwa wakulimambalimbali hapa nchini il kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula hapa nchini na hivyo kukabiliana na upungufu uliopo wa bidhaa hiyo.”amesema Kanali Lushika

Kwa mujibu wa Kanali Lushika ,katika pango wa 2022/23 JKT limepanga kulima ekari takriban 1,700 za mbegu za alizeti aina ya Recors katika vikosi mbalimbali vya JKT ambayo imefanyiwa utafiti na kuonyesha inatoa mafuta mengi.

Aidha amesema,mpango wa JKT kwa mwaka 2023/24 ni kufungua mashamba makubwa ya mbegu ya alizeti takribani ekari 5,000 ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Naye Kaimu Kamanda wa kikosi cha 834 KJ Makutopora Meja James Macheta amesema katika eneo hilo kuna shamba la ukubwa wa ekari 1,000 na lilianza kuandaliwa Oktoba na kupandwa mwezi Disemba, 2022 na ekari 200 zimelimwa katika Wilaya ya Kongwa.

Katika hatua nyingine amesema uzalishaji katika mashamba hayo vijana wa kujitolea wameshirikishwa kwa asilimia 100 katika ngazi zote ikiwa ni kuwajengea uwezo na kuwapa ujuzi.

Abdul Mmasi ni miongoni mwa vijana wa JKT ambaye amesema ,kupitia kilimo hicho cha alizeti ameweza kujifunza mambo mengi ambayo yatamsaidia katika shughuli za kilimo pindi atakapohitimu mafunzo ya JKT na kurejea uraiani.