November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JKCI yaipa tuzo NHIF ugharamiaji matibabu ya moyo kwa Watanzania

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online, Zanzibar

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umepongezwa na kutunukiwa tuzo kutokana na mchango wake wa kugharamia matibabu ya Moyo kwa wanachama wake hatua iliyowezesha kuboresha huduma kwa wananchi wote hususan kwa magonjwa ya moyo.

Tuzo hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki Zanzibar kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo uliofunguliwa na Makamu wa Rais Dkt. Philipo Mpango.

Tuzo hiyo ilitolewa na Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kutambua mchango unaotolewa na NHIF katika kugharamia huduma za matibabu ya moyo.

Akizungumzia tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu NHIF, Dkt. David Mwenesano, alisema kitendo cha NHIF kugharamia huduma za moyo kunaziwezesha hospitali kuendelea kuboresha huduma.

“Kwa kugharamia huduma hizo, mapato yake yanawezesha uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba lakini inachochea kupatikana kwa Wataalam wabobezi wa magonjwa ya moyo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
Alisema kuwa NHIF inaendelea kushirikiana na Watoa huduma kuhakikisha mazingira ya utoaji wa huduma kwa wananchi yanakuwa bora zaidi.