November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JKCI yafanya upasuaji watoto 427

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

TAASISI ya moyo ya jakaya kikwete (JKCI) imeendesha kambi maalumu ya siku tano ya uchunguzi na upasuaji kwa watoto 427 wenye matatizo ya matundu kwenye moyo, matatizo ya mishipa ya damu na valvu za moyo

Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo mkurugenzi wa upasuaji kutoka taasisi ya Jakaya kikwete Dkt. Angela Mhozya alisema kuwa kambi hiyo imefanikisha upasuaji mkubwa kwa watoto 18 na upasuaji kwa njia ya tundu dogo kwa watoto 41 huku akishukuru shirika la Muntada aid kwa kuwezesha kambi hiyo

““Hawa ni madaktari ambao wamekuwa wakija katika Taasisi ya moyo kwa miaka saba mpaka sasa na wanakuja kwa ajili ya matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto na kwa kawaida wakija huwa tunafanya uchunguzi kwa watoto wengi na wengine wanapitiwa huduma za upasuaji,”

“Tunawashukuru sana wenzetu kwa kuendelea kufanya kazi na JKCI kwanza wanatujengea uwezo kila mwaka tunaenda hatua mbele na pia wanatuletea vifaa katika kila walichotuelekeza wakirudi tumepiga hatua zaidi,”alisema Dkt. Mhozya

Kwa upande wao wawezeshaji wa kambi hiyo kutoka mradi wa little heart alisema kuwa tafiti zimebaini kuwa asilimia 90 watoto wanaozaliwa na matatizo ya moyo katika la bara la afrika hawapatiwi matibabu stahiki na kuongeza wataendelea kushirikiana na madaktari wa nchi za afrika ili kuokoa maisha ya watoto wengi zaidi.

Naye mmoja wa wazazi walionufaika na progamu hiyo Diana Kurwa aliishukuru serikali na taasisi ya moyo ya jakaya kikwete kwa kugharamia sehemu kubwa ya matibabu ya mtoto na kuwataka wazazi wengine wenye watoto wenye matatizo ya moyo kufika katika taasisi hiyo ili kujipatia huduma hizo