January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jimbo la Mbeya wajitokeza kumpokea Tulia Ackson

Na Esther Macha,TimesMajira Online,Mbeya

BAADHI ya wananchi wa Jiji la Mbeya wakiongozwa na madereva Bodaboda wamejitokeza kumpokea Mbunge wa Mbeya Mjini na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Dkt Tulia Ackson wakati akiwasili kutokea Dodoma baada ya kumaliza shughuli za Bunge.

Mapokezi hayo yalianzia Kata ya Nsalaga kwa maandamano ya Bodaboda na magari na kuhitimishwa kwa mkutano mfupi wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa ndege wa zamani uliopo Kata ya Iyela.

Awali Paul Christopher kwa niaba ya viongozi wa Kanda alitumia nafasi hiyo kumpongeza Dkt Tulia kwa uwakilishi mzuri katika vikao vya Bunge sambamba na kuwasemea wananchi wa Mbeya.

“Kama mwanachama wa Bodaboda tumeshukuru kututetea kuhusiana na fani za Bodaboda kutoka shilingi elfu thelathini hadi shilingi elfu kumi”amesema Christopher.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodaboda Jiji la Mbeya ,Aliko Fwanda amesema baada ya madereva wa Bodaboda kulalamikia faini kubwa wanazotozwa barabarani alimwendea mbunge na kumweleza changamoto hiyo ambapo Mbunge bila hiyana aliiwasilisha Bungeni hatimaye kupitishwa.

“Hii inaonesha namna mbunge alivyo makini kwa kusikiliza kero za wananchi na kuzifikisha sehemu husika “amesema Fwanda.

Hata hivyo kiongozi huyo wa boda aliwataka vijana kuacha maneno bali wachape kazi kwa bidii ili kujiongezea kipato.

Aidha katika hotuba yake Dkt.Tulia aliwashukuru wananchi kwa mapokezi makubwa ambayo hakuyatarajia.

“Mapokezi haya yananipa ari ya kuwatumikia wananchi na nichukue fursa hii kuwajulisha kuwa mambo yaliyopitishwa Bungeni nitawaeleza katika mikutano yangu”amesema Tulia huku vijana wakishangilia.

“Hizi ni mvua za rasharasha mmejionea ukarabati wa barabara za pembezoni ujenzi wa zahanati na mambo mengine mtambue kuwa serikali ya awamu ya sita ipo kazini.

Alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassani kwa kukubali kuwapunguzia tozo za barabarani inaonesha namna Rais anavyowajali wanyonge wakiwemo waendesha Bodaboda.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wa Chama Cha Mapinduzi Jiji la Mbeya.