November 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JIKOKOA washiriki mjadala wa kitaifa wa Nishati safi ya kupikia

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameielekeza wizara ya Nishati inayoongozwa na Waziri January Makamba kuhakikisha ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mapema mwaka 2023, nishati safi inasambazwa kwenye taasisi kubwa.

Rais Samia aliyasema hayo, wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la Nishati Safi ya Kupikia ‘Tanzania Clean Cooking, Conference’ lililofanyika jana, jijini Dar es Salaam.

“Wakati nikiwa Makamu wa Rais, na nina bahati na January kwenye mambo ya mazingira. Kule nilimuelekeza taasisi zinazohudumia zaidi ya watu 300 lazima watumie nishati safi… akiwa kule hakukaa muda mrefu akatoka hatukulitekeleza. Nakuelekeza tena leo, lilelile kwamba taasisi zile; jela, shule, vikosi vya ulinzi zianze sasa kujielekeza kwenye nishati safi ya kupikia.” ameagiza Rais Samia

“Nimemsikia hapa Dada yangu Tibaijuka akisema katika kitabu chake alichokiandika kwamba alisisitiza umuhimu wa kupanda miti ya mkaa, sasa mimi nataka kubadili fikra tupande miti ya matunda maana hiyo huwezi kuikata bila sababu maalum, tuwahimize watu watumie nishati safi ya kupikia,” amesisitiza Rais Samia.

Aidha Rais Samia aliitaka Wizara ya Nishati kuhakikisha inahamasisha matumizi hayo ya nishati safi ya kupitia kwa taasisi mbalimbali nchini ikiwemo Magereza, Mashule na Maofisini ili kupunguza matumizi ya mkaa ambao unapatikana kutokana na miti ambayo husaidia uhifadhi wa mazingira.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Biashara Afrika Mashariki, Irene Kamande anaye jishughulisha na uuzaji wa jiko la mkaa na kuni liitwalo Jikokoa alisema Majiko yao yanatumia mkaa na kuni chache na hayana madhara kwa mtumiaji kwasababu hewa mbaya ambayo inatoka inakua siyo nyingi kama ile ambayo inatoka kwenye jiko la kawaida.

Alisema Majiko yao yanapatikana kwa bei ya chini ambayo kila mtanzania anaweza inunua lakini pia yanatumia mkaa mdogo sana ambapo kwa mwezi mtu anaweza kutumia gunia zima lakini kwa kutumia majiko hayo mtu atatumia 30% tu ya mkaa.

“Kwa sasa tumeweka bei ambayo imesaidia kuongeza soko kwa kuuza majiko kwa wingi, ambapo tumesambaza majiko katika mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha na kwa sasa tupo Dar ambapo Mbeya na Mwanza tutafika pia”

Kuhusu kuongeza Ajira kupitia biashara hiyo, Kamande alisema wameajiri watu zaidi ya 100 na mpaka kufikia mwaka 2023 wanampango wa kuongeza ajira kwa watu takribani 2000.

“Jiko okoa imesaidia sana kuongeza fursa za ajira na sasa tumeshaajiri watu takribani 100 na hadi kufikia mwezi Disemba tutakua tumeajiri watu zaidi ya 500 na matarajio yetu hadi kufikia mwaka mmoja ujao tutaajiri watu 2000”

Mbali na hayo, Kamande aliiomba serikali wapunguze masharti ambayo wameyaweka kwani majiko hayo wanayalipia ushuru mkubwa ambapo ikitokea bei wakaipandisha watumiaji wa majiko hayo watashindwa kununua bidhaa hiyo.

Aidha aliwataka Wananchi kutumia jikokoa kwani litaokoa pesa na afya.