Na Penina Malundo, timesmajira
Taasisi nne zinazounda Jeshi la Uhifadhi chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii zimeagizwa kuhakikisha zinashiriki kikamilifu katika kudhibiti changamoto za wanyamapori wakali na waaribifu nchini na kuwa suala hilo si la taasisi moja tena kama ilivyo kuwa sasa.
Agizo hilo limetolewa Jijini Arusha na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna Benedict Wakulyamba kwenye ufunguzi wa warsha kwa Makamishna na Maafisa wa Uhifadhi yenye lengo la kupata kukumbushana masuala mbalimbali ya uhifadhi pamoja na masuala ya haki za kibinadamu.
Kamishna Wakulyamba amesisitiza kuwa Jeshi la Uhifadhi kuchukulia changamoto hiyo ya wanyamapori wakali na waharibifu kuwa ni suala la dharura na kuwa mpango kazi wa kwanza wa kila Taasisi iwe ni ya kupanga kukabiliana na changamoto hiyo.
Aidha, Kamishna Wakulyamba amewaelekeza Makamishna wote wa Jeshi hilo kuhakikisha Jeshi la Uhifadhi linakuwa la mfano katika kutekeleza majukumu yake, kwakuwa na Watumishi wenye nidhamu na weledi wa hali ya juu na kusisitiza kuwa, yeyote atakaeishi kinyume na Jeshi hilo ajue kuwa hilo ndilo anguko lake Mwenyewe.
“Ndio maana tumekuja na hii warsha, ili tupeane miongozo, tukumbushane, tukitoka hapa ukifanya kinyume hayo ya kwako kwa kuwa sisi hatukutuma wala kukuagiza, na niimani yangu kuwa mtautumia muda wenu vizuri kuwasikiliza wawezeshaji wetu katika maeneo mbalimbali” amesisitiza Kamishna Wakulyamba.
Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Kitengo cha Uratibu wa Jeshi la Uhifadhi Kamishna Msaidizi Fidelis Kapalata ameeleza kuwa Semina hiyo ya siku tano inayowahusisha Viongozi wa Jeshi la Uhifadhi, inakusudi la kuwakumbusha masuala mbalimbali ya usimamizi wa wanyamapori, Misitu, usimamizi wa Rasilimali watu na masuala mengine mbalimbali.
Maafisa hao wa Jeshi la Uhifadhi pamoja na mambo mengine, wanatarajia kujifunza kuhusu Afya ya akili na msongo wa mawazo, Mahusiano na mawasiliano mahala pa kazi, Nafasi ya Maadili na Mabadiliko katika Utamaduni kwa Usimamizi bora wa Maliasili na Utalii, Utatuzi wa Migogoro na Maridhiano, Mapambano dhidi ya Rushwa mahali pa kazi nk.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato