November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jeshi la Polisi kuimarisha usalama mikoa ya mipakani

Na Moses Ng’wat, Songwe.

JESHI la Polisi nchini limeeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha hali ya ulinzi na usalama katika mikoa ya mpakani ili kukabiliana na changamoto ya uingizwaji wa bidhaa za magendo.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime, amebainisha hayo Januari Mosi, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari wa Mkoa wa Songwe mara baada ya kumaliza ziara ya siku mbili mkoani humo.

Ziara hiyo ilikuwa mahususi kwa ajili ya ukaguzi na kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo Maofisa, Wakaguzi, Askari wa vyeo mbalimbali pamoja na wananchi kuhusu ushirikiano katika kubaini na kuzuia uharifu.

Misime ametaja mikakati hiyo kuwa ni kuweka wakaguzi wa polisi kila kata kwenye Miji iliyopo maeneo ya mikoa ya mpakani, pamoja na kutoa elimu kwa wakazi wa maeneo hayo juu ya namna watakavyoweza kutoa taarifa za uhalifu ikiwemo biashara haramu za magendo.

Hivyo,  Misime amewaomba wananchi kuendeleza ushirikiano na jeshi hilo katika kutoa taarifa zenye viashiria vya uhalifu katika maeneo yao.

Ametaja mkakati mwingine ni jeshi hilo ni kuendelea kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba mipaka inaendelea kuwa salama pamoja na kudhibiti biashara za magendo kwa kiwango kinachostahili kwa mujibu wa sheria.

Aidha ameeleza kuwa, pamoja na mikakati hiyo, jeshi limeendeleza ushiriakiano na nchi jirani katika kuimarisha hali ya usalama mipakani kwa kufanya mikutano ya pamoja, ikiwemo  ubadilishanaji wa taarifa za kiuhalifu kati ya Tanzania na nchi hizo.

“Tunafanya mikutano ya mara kwa mara kuhakikisha tunapeana taarifa mbalimbali za  kuweza kubaini na kuzuia uharifu, lakini pia kama kuna uharifu umetokea na labda waharifu wakakimbilia nchi nyingine basi tunashirikishana na wanakamatwa,” amesisitiza Misime.