Na. Mwandishi Wetu, Longido
Jeshi la Polisi mkoani Arusha litaendelea na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto kwa kuhakikisha wanaibua na kuwachukulia hatua watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Hayo yamesemwa na Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake (TPF NET) mkoani humo Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Edith Swebe wakati akiongea na wananchi wa Jamii ya wafugaji, Namanga Wilayani Longido katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili.
SSP Swebe amesema ni wakati sasa wa jamii kuwaibua na kuwafichua watu wachache wanaofanya vitendo hivyo vya ukatili katika jamii ambapo Jeshi la Polisi litaendelea kufanya doria pamoja na kutoa elimu kuanzia ngazi ya familia, mtaa, Kata na hata wilaya ili kuhakikisha matukio ya ukatili yanaisha kabisa
Sambamba na hilo pia amesema Jeshi la Polisi limeungana na jamii hiyo ili kujenga mshikamano wa pamoja katika kuibua na kupinga vitendo hivyo ambapo ametoa wito kwa Wananchi kufika mahakamani kutoa ushahidi dhidi ya watuhumiwa wa matukio hayo ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao.
Naye kaimu katibu Tawala wa Wilaya ya Longido kwa Niaba ya Mkuu wa Wilaya Bwana Boniphace Lugola amewataka wananchi, viongozi wa vitongoji, vijiji na Watendaji wa ngazi zote kila mmoja kwa nafasi yake kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kufuatilia na kuwafichua wahalifu wote wanaojihusisha na matukio ya ukatili katika jamii wanazoishi.
Pia ametoa rai kwa Jeshi la Polisi kukamilisha upelelezi wa makosa ya ukatili kwa wakati na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Mkuu wa Polisi wilaya ya Longido Mrakibu wa Polisi SP Leah Ncheyeki amesema Jeshi la Polisi Wilayani humo lilipata mafanikio ambapo jumla ya kesi 36 zilipata mafanikio mahakamani na watuhumiwa kupatikana na hatia na kuhukumiwa.
Pia amesema jamii wilayani humo imepata elimu kuhusina na vitendo vya ukatili wa kijinsia ambapo kupitia elimu hiyo wananchi wengi wanafika katika vituo vya polisi kuripoti matukio ya ukatili ukilinganisha na miaka iliyopita ambapo jamii ilikua inaficha matukio hayo
Kwa upande wa wakina mama wa eneo la Namanga wamesema hapo awali katika eneo hilo walikua na changamoto kubwa ya matukio ya ukatili wa kijinsia lakini kupitia Jeshi la Polisi matukio hayo yamepungua kwa kiasi kikubwa kupitia elimu mbalimbali inayotolewa.
More Stories
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni