November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jengo la JJ lateketea kwa moto

Na Suleiman Abeid,Timesmajira Online, Shinyanga

MOTO ambao haujafahamika chanzo chake umeteketeza sehemu kubwa ya jengo linalomikiwa na Jumuiya ya Wanawake wa Tanzania (UWT) mkoani Shinyanga maarufu jengo la J.J na kusababisha hasara kubwa kwa wamiliki wa maduka wanaopanga kwenye jengo hilo.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga, Martine Nyambala.

Katibu wa UWT Mkoa wa Shinyanga, Asha Kitandala amesema moto huo umetokea usiku wa kuamkia leo mnamo saa 9.20 na kwamba yeye alipata taarifa baada ya kupigiwa simu na walinzi wa kampuni ya Tigo hivyo akamtaarifu Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga.

“Tunahisi chanzo cha moto huu ni hitilafu ya umeme, tumeoneshwa eneo ambalo inadaiwa ndipo ulipoanzia, lakini ki ukweli ushirikiano wa watu wa Zimamoto ni hafifu, wamechelewa kufika eneo la tukio, inadaiwa walifuatwa mapema lakini hawakufika kwa wakati,”amesema Kitandala na kuongeza kuwa

“Mimi nimepigiwa simu saa 10 usiku, ninaishi mbali kule eneo la Mwasele hivyo nilipopata taarifa nilimtaarifu pia Katibu wangu wa Mkoa wa CCM, tukafika hapa tukakuta Zimamoto wanaendelea kuzima moto, walinzi waliokuwepo hapa wametusaidia, na ndiyo waliowafuata Zimamoto ofisini kwao,”..

Mmoja wa wafanyabiashara ambao ni wapangaji kwenye jengo la J.J (kulia) akihojiwa na mmoja wa maofisa wa Shirika la TANESCO mkoani Shinyanga juu ya tukio hilo la moto.

Baadhi ya wamiliki wa vyumba vya biashara vilivyoteketea na moto kwenye jengo hilo wamesema hasara ambayo wameipata ni kubwa na kwamba iwapo Kikosi cha Zimamoto kingewahi kufika eneo la tukio huenda moto huo ungedhibitiwa kabla haujasababisha madhara makubwa.

Mlinzi wa Kampuni ya ulinzi ya SGA anayelinda jengo la Ofisi za TIGO Mjini Shinyanga Birega Silvanus amesema akiwa katika eneo la lindo lake mnamo saa 9.20 usiku alisikia mlipuko wa kitu kama hitilafu fulani ya umeme lakini hata hivyo mwanzoni hakufuatilia.

“Lakini baada ya muda kidogo kama dakika tano hivi nikaona moshi umetanda juu ya jengo hilo hivyo nilishuka chini kwenda kuangalia nini kimetokea, nikakuta moto unawaka, na upande ule wa gesti palikuwa na akinamama ambao walianza kupiga kelele za kuomba msaada,”ameeleza Silvanus na kuongeza kuwa

“Kwa haraka haraka nilichukua bodaboda na kwenda ofisi za Zimamoto nikawaeleza kwamba kuna tukio la moto, wakasema wanakuja na mimi nikarejea kwenye lindo langu, baada ya kama dakika 28 hivi ndipo Zimamoto walifika hapa na kuanza kuzima moto huo,”.

Eneo ambalo linahisiwa kutokea hitilafu na kusababisha jengo la J.J kuteketea kwa moto.

Johari Ramadhani mmiliki wa Salon ya kusuka nywele amesema alipigiwa simu kutaarifiwa kuhusu moto huo mnamo saa 9.30 usiku kwamba jengo la J.J,linateketea kwa moto na alipofika alikuta tayari moto umeishazimwa lakini kila kitu ndani ya salon yake kimeteketea.

Naye mwangalizi wa nyumba ya kulala wageni iliyopo kwenye jengo hilo ambapo hata hivyo moto huo haukuathiri upande wa vyumba, Lucia Faustine amesema mnamo saa tisa usiku kabla ya kutokea tukio la moto alimpokea mteja mmoja na kumpatia chumba.

Hata hivyo anasema muda mfupi baada ya kama dakika 15 baada ya kumuhudumia mteja huyo alisika kelele nje na alipotoka kutaka kufahamu kilichotokea alikuta moto unawaka kwenye jengo la mbele hivyo aliwaamsha wapangaji wake wote watoke nje kwa vile kuna moto unawaka.

Kwa upande wake mmiliki wa duka kubwa lililokuwa kwenye jengo hilo ambalo kwa sehemu kubwa ndilo limeteketea kwa moto aliyejitambulisha kwa jina moja la Frank amesema alipata taarifa ya moto mnamo saa 9.30 usiku na akafika eneo la tukio na kukuta tayari moto unaendelea kuwaka.

“Nilipigiwa simu mnamo saa 9.30 usiku nikaja hapa nikakuta tayari moto unawaka, tuliwataarifu Zimamoto lakini walichelewa kufika katika eneo la tukio, hivyo moto ulienea katika jengo lote na mimi vitu vyangu vyote vimeteketea kwa moto, takriban zaidi ya mali zenye thamani ya shilingi milioni 47 zimeteketea,” ameeleza Frank.

Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoani Shinyanga, Mrakibu Martine Nyambala amekiri kutokea kwa tukio hilo la moto katika jengo la J.J. lililopo Mjini Shinyanga barabara ya Uhuru na kwamba askari wa kikosi hicho wamejitahidi kuudhibiti moto huo kabla haujaenea kwenye majengo jirani.

Amesema mara baada ya kupata taarifa ilibidi Askari wa Zimamoto wawahi eneo la tukio na kwamba madai ya kuchelewa kufika katika tukio hayana ukweli kwa vile wanapopokea taarifa lazima wajiandae kwa haraka ikiwemo kuwashwa kwa gari ambalo huchukua takribani dakika kadhaa kuwa katika hali ya kufanya kazi.

“Mnamo saa 9.51 usiku hivi tulipokea taarifa ya tukio la moto eneo la mjini kati jirani na Ofisi za TRA Mkoa wa Shinyanga, na baada ya muda si mrefu askari wa Zimamoto walifika eneo la tukio, bahati mbaya walikuta tayari moto umeisha enea sehemu kubwa ya maduka ukiwaka,”

“Katika eneo hilo pia kuna nyumba ya kulala wageni, moto ulikuwa umeishaenea upande wa maduka, lakini wapiganaji walifanikiwa kuudhibiti usienee kwenye maeneo mengine ya nyumba ambapo walifanikiwa kuokoa maduka sita kati ya maduka 13 yaliyopo kwenye jengo hilo, maduka saba yalikuwa yameteketea,” ameeleza Kamanda Nyambala.

Kamanda huyo ametoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Shinyanga kwamba panapotokea tukio la moto, jambo la kwanza ni kupiga namba ya dharura kwenye kikosi cha Zimamoto ambayo ni 114 badala ya kuwapigia watu wengine na kwamba dakika tano kwenye tukio la moto ni nyingi sana kwa vile moto husambaa kwa haraka.

“Mfano mzuri tukio hili la hapa J.J. mtu wa kwanza kuliona kwanza alimpigia simu mmiliki wa duka, hivyo mpaka alipokuja kufika hapa na kutoa taarifa Zimamoto tayari moto ulikuwa umeenea sehemu kubwa ya jengo, ilibidi kabla ya kumpigia mmiliki wangepiga simu katika kikosi cha Zimamoto ili tuweze kuwahi,” ameeleza.

Kamanda Nyambala amesema mpaka sasa wanaendelea na uchunguzi wa kina ili kuweza kubaini chanzo cha moto huo.

Huku mmoja wa watumishi wa Shirika la Umeme TANESCO Siraji Msagati amesema baada ya kupata taarifa za moto waliwahi na kukata umeme kwenye eneo lote la tukio.

“Tunaamini moto huu chanzo chake hakijafahamika maana siyo kweli kwamba ni hitilafu ya umeme, maana tulipofika hapa tulikuta umeme ukiendelea kuwaka, hivyo tulichukua hatua za kukata umeme maeneo yote kabla moto haujasambaa eneo kubwa, nafikiri ni hitilafu nyingine tu siyo umeme,” ameeleza Msagati.