Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Sengerema
Mahakama ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, imemuhukumu kifungo cha miezi sita Rajabu Reli (22), mkazi wa Sengerema baada ya kukutwa na hatia ya kuvaa sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) bila ruhusa.
Hukumu hiyo imetolewa, Januari 7,2025 katika shauri la jinai namba 445 la mwaka 2025 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Evodius Kisoka, mbele ya Mwendesha mashtaka wa Serikali Nyamhanga Tissoro.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa na Mwendesha mashtaka wa Serikali Nyamhanga Tissoro mbele ya Hakimu Evodius Kisoka, mshtakiwa alitenda kosa hilo mnamo Desemba 05,2024, huko kijiji cha Kasisa, Wilaya ya Sengerema, kinyume na kifungu cha 178(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.
Mshtakiwa alifikishwa mahakamani Januari 07,2025 na kusomewa shitaka la kuvaa sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania bila ruhusa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada ya kusikiliza pande zote za ushahidi Hakimu Evodius Kisoka alijiridhisha kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri ni mzito na haukuacha shaka lolote.
Hata hivyo, mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujitetetea kwanini asipewe adhabu, aliomba Mahakama hiyo imuachie huru kwa kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na alivaa ili akubaliwe na mchumba wake.
“Hakimu naomba nisamehewe kwa kuwa ni kosa la kwanza na niliva,kwenda kumuonesha mchumba wangu kuwa mimi ni Askari ili asinikatae,”aliomba Rajabu
Ombi hilo lilitupiliwa mbali na Hakimu Kisoka na kutoa hukumu hiyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama ya Rajabu.
More Stories
Wananchi Kisondela washukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango
LALJI yatoa msaada wa sare na vifaa vya shule kwa yatima