October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jela maisha kwa kumlawiti mtoto

Na Allan Vicent, TimesMajira Online,Tabora

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi mkoani Tabora imemhukumu kijana, Benard Meshack (26) kifungo cha maisha jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumfanyia ukatili wa kijinsia mtoto mwenye umri wa miaka minne.

Adhabu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Jovin Kato baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo juu ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili kijana huyo za kufanya mapenzi kunyume cha maumbile na mtoto mdogo ambaye jina lake linahifadhiwa.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Kato amesema, baada ya mahakama kusikiliza maelezo ya pande zote mbili imeridhika pasipo shaka kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo la kinyama na kubainisha kuwa adhabu inayostahili kwa kosa hilo ni kifungo cha maisha.

Awali upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili msomi Tito Mwakalinga umeieleza Mahakama kuwa, mshitakiwa alitenda kosa hilo Julai 02, 2020 alipokuwa amemfuata mtoto huyo shuleni ili kumrudisha nyumbani.

Wakili Mwakalinga ameongeza kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 154 (1) (a) na (2) cha sheria ya makosa ya jinai Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Wakili Mwakalinga amedai kuwa, mshitakiwa huyo ambaye aliaminiwa na kukabidhiwa mtoto ili kumpeleka shule na kumrudisha nyumbani kila siku, siku ya tukio baada ya kumtoa shule alimpeleka nyumbani kwake na kisha kumfanyia ukatili huo huku akijua kuwa ni kosa.

Baada ya mahakama kumtia hatiani upande wa mashitaka uliomba apunguziwe adhabu kwa kuwa hilo ni kosa lake la kwanza na ni kinyume na maadili ya Watanzania na pia linaenda kinyume na imani za dini zote hapa nchini ndipo Hakimu Kato akamhukumu kifungo cha maisha jela.

Baadhi ya wananchi waliokuwepo mahakamani hapo walielezea kusikitishwa na kitendo kilichofanywa na kijana huyo hasa ikizingatiwa kuwa, dunia nzima imekuwa ikipigia kelele vitendo vya namna hiyo huku ikiitaka jamii kujiepusha na ukatili au unyanyapaa kwa akinamama na watoto.