Na Philemon Muhanuzi
NIMESIKILIZA nyimbo mbili tatu kuhusu ugonjwa hatari wa Corona, kwa kweli ni za kusikitisha. kwani zimejaa mashairi ya huzuni, yenye kuuongelea mateso ya maradhi haya.
Lakini zimekuwa ni nyimbo ambazo video zake za mitandaoni, zimejumuisha matukio yenye kuonyesha shughuli nzito wanayofanya madaktari pamoja na manesi.
Na ni shughuli yenye kuonyesha namna baadhi ya wanadamu wanavyozaliwa na ile nia ya upendo wa kujitoa kwa faida ya walio wengi.
Nia ya kibinadamu isiyoweza kuhongwa au kununuliwa na mtu kwa kutumia pesa zenye kushikika kwa mkono.
Hizi zimekuwa ni nyakati za watu wa sekta afya kuonekana wakiwa wamevaa mavazi yao meupe na mdomoni wamejikinga na barakoa.
Nyakati ambazo manesi wanauguza wagonjwa mahospitalini wakijiweka kwenye hatari ya kuupata ugonjwa huo.
Wakati bado Corona haijaanza kuwa na madhara mazito haswa katika mataifa ya Ulaya, alisikika daktari mmoja akihoji nani ni wa muhimu kati ya mwanamichezo anayelipwa mamilioni ya pesa na mhudumu wa afya.
Wanamichezo waliisikia kauli ile popote walipo dunia nzima, hawakuweza kuijibu. Kilichotokea siku kadhaa baada ya kauli ya huyo daktari kikawa ni ushahidi wa ukweli wa maneno yake.
Kwamba dunia nzima ikiwa na afya njema, ndipo ushangiliaji wa Cristiano Ronaldo unapoweza kuigwa hata na watoto wadogo wa Burundi na Chile.
Kwamba katika nyakati ambazo barakoa inaonekana ni muhimu ndani ya vyumba vya upasuaji, ndipo mjadala wa mshahara wa Lionel Messi unapamba moto katika njia mbalimbali za mawasiliano.
Mamlaka za Uingereza zimemshangaa Jose Mourinho na baadhi ya wachezaji wa Tottenham Hotspurs kuweza kudiriki kutoka nje na kufanya mazoezi pembeni ya barabara za huko Uingereza.
Hiki ni kipindi ambacho runinga hazihitaji kumuona mwanasoka akifanya mazoezi kana kwamba hewa inayomzunguka ni safi kabisa kiasi cha kukosa virusi vya Corona.
Wenye kuamini nadharia za namba ya miaka wanajenga hoja kuwa miaka inayoishia na namba 20 huwa haipiti pasipo majanga ya kidunia kuwepo.
Wakikumbushia homa ya mafua iliyotesa dunia kuanzia 1918-20, pia wakikumbushia dhahama nyingine za karne zilizopita. Umuhimu wa afya umekuwa ni somo la bure kabisa mwaka huu.
Tumekumbushwa kuwa hata huyo mwanamichezo tunayemfuatilia katika kurasa zake za mitandao, kuna siku mwisho wa matembezi yake unaweza kuwa ni mle ndani ya nyumba yake.
Hayo mamilioni anayolipwa ambayo yameandikwa katika mikataba, kuna siku yanaweza kuwa ni kama makaratasi tu ikiwa atajisahau na kuambukizwa maradhi ya Corona.
Tunakumbushwa kuwa virusi vya Corona ambavyo haviwezi kuonekana kwa macho pasipo darubini maalum, vina nguvu ya kusimamisha ratiba za ligi mbalimbali.
Yale majukwaa maarufu wa uwanja wa Old Trafford kwa sasa yapo kimya kabisa, ukikaa katika kiti kimojawapo kwa sasa unaweza kudhani upo katika eneo la makaburi saa sita usiku.
Yale majukwaa maarufu ya uwanja wa Nou Camp kwa miezi hii ya Corona yamekuwa ni sehemu ya upweke. Kirusi kimoja tu kimemkumbusha mpenda michezo umuhimu wa afya kuwa ni njema.
Katikati ya mwaka huu michuano ya EURO 2020 ilitarajiwa kufanyika, ikiwa ni utaratibu ule ule wa kila miaka minne kufanyika mara moja.
Lakini kimeibuka kirusi hatari na shirikisho la soka barani Ulaya UEFA, imebidi wabadili ratiba nzima.
Mengi ambayo yameshatokea tangu daktari yule akumbushe umuhimu wadau wa sekta ya afya kulipwa pesa nyingi kulingana na mazingira hatarishi ya kazi yao.
Na hayo mengi yamethibitisha kwamba alichosema kilikuwa ni ukweli. Afya zetu zinapokuwa bora tunapata ujasiri wa kuwadharau watu muhimu kuliko wanamichezo wote kwa ujumla.
Wanachokifanya wanamichezo katika kutoa mchango wa hali na mali kwenye mapambano dhidi ya Corona ni jambo la kheri sana.
Lakini ugonjwa huu ni kama umekuja ili kumkumbusha binadamu kuwa asikufuru na kujiona anao utawala mkubwa juu ya maisha yake.
Baadhi wanasema kusema kwanini ujumbe huu mzito umekuja mwaka huu wa 2020 na sio miaka ya nyuma?.
Ratiba za anayetuumba sio kama zile ratiba za muda wa chakula cha mchana na usiku tunazojiwekea majumbani mwetu.
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
Miaka 63 ya Uhuru na rekodi treni ya SGR