January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jamii yatakiwa kuwalinda watoto kuliko mali

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii Dkt.Dorothy Gwajima ameitaka jamii kuhakikisha inawalinda watoto dhidi ya ukatili kuliko hata inavyolinda mali zao nyingine.

Dkt.Gwajima ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Familia ya Kimataifa iliyoenda sambamba na uzinduzi wa Kampeni kuhusu mmomonyoko wa maadili .

Amesema moja ya changamoto inayosababisha uwepo wa watoto wa mitaani ni wazazi kutowajali na kuwalinda watoto kama wanavyolinda mali zao.

“Katika jamii tunakoishi,utakuta baba akiibiwa kitu chake cha thamani au ng’ombe wake ataenda kutoa taarifa hadi polisi,lakini leo tunaona kuna watoto wanaishi huku mitaani wazazi wao wako wapi,hii ni kutokana na kutojali kitu ambacho hakifai kwa ustawi wa watoto wetu hapa nchini.”amesema Dkt.Gwajima

Amesema kila mzazi na mlezi atimize wajibu kikamilifu katika kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya ukatili lakini pia kuwawekea mipaka katika matumizi ya utandawazi .

“Watoto tunawaacha wanaangalia TV kadri wanavyotaka,lakini pia tunawaacha wanatumia simu za zetu za mkononi,lazima mzazi uwangalie na kumdhibiti mtoto na kumwekea mipaka ili atumie utandawazi katika kujifunza mambo yanayofaa na siyo vinginevyo.”amesisitza Waziri huyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Fatma Tofiq amesisitiza maadili mema katika jamii na upendo ndiyo nguzo  ya kuondokana na vitendo vya ukatili .

“Tukiwa na maadili lakini pia tukipendana lazima tutaondosha vitendo hivi vya ukatili hasa katika familia .

Naye Mchungaji Richard Hananja amesema jamii inapaswa kuthaminiana pamoja na kuwa hofu ya Mungu ili kuondokana na vitendo vya ukatili.

“Thamani ,kila mmoja akiona uthamani wa mwenzake hali ya kukatiliana itaondoka ,kwa sababu huwezi kumfanyia ukatili mtu unayemwona ni wa thamani kwako.”amesema Mchungaji HananjaAwali Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt.John Jingu ameiasa jamii kutumia muda wa kutafakari na kuitumia siku hiyo kama sehemu ya kukaa na familia kutafakari na kuona namna ya kia mtu kutimiza majukumu yake katika ulezi wa familia