January 17, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jamii yashauriwa kuzingatia ulaji bora, vyakula vya asili

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Imeelezwa kuwa magonjwa yasiyoambukiza yanaongezeka kwa kasi ambapo yanaathiri hata watu wenye umri mdogo wakiwemo watoto.

Ambapo nchini hapa kulingana na utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO)ni kuwa Mwaka 1990 vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyoambukiza vilikuwa asilimia 19 na 2015 vikaongezeka mpaka asilimia 34.

Ili kukabiliana na changamoto hiyo,wito umetolewa Kwa jamii kuzingatia ulaji unaofaa kwa kula vyakula vya asili pamoja na ufanyaji wa mazoezi.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Chama cha ugonjwa wa Kisukari Tanzania Profesa Andrew Swai, akiwasilisha mada katika mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uelewa wa waandishi wa habari kutoka mikoa ya Kanda juu ya namna ya kuripoti habari zinazohusu magonjwa yasiambukiza yaliofanyika jijini Mwanza.

Profesa Swai, ameeleza kuwa
magonjwa yasiyoambukiza,hayana vimelea vinavyoweza kusambazwa ambapo magonjwa hayo ni pamoja na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu,saratani,magonjwa sugu ya njia ya hewa,kisukari,magonjwa ya akili,ajali pamoja na selimundu.

Ameeleza kuwa magonjwa hayo yanaongezeka kwa kasi ambapo asilimia 71 ya vifo vyote duniani kwa mwaka 2016 vilitokana na magonjwa yasiyoambukiza huku asilimia 75 ya vifo vyote vya watu wenye miaka 30-70 husababishwa na magonjwa hayo.

Pia ameeleza kuwa,visababishi vya magonjwa hayo ni pamoja na ulaji usiofaa na matumizi ya vilevi,kutoushughulisha mwili,kuketi mfululizo kwa muda mrefu,msongo wa mawazo,kutopata usingizi wa kutosha na matumizi ya tumbaku.

“Jamii inapaswa kuzingatia ulaji unaofaa na kuachana na ulaji mbaya,matumizi ya tumbaki pamoja na kufanya mazoezi kwani magonjwa haya hayana tiba,”ameeleza Profesa.Swai.

Mtaalamu wa Mawasiliano kutoka Chama cha Kisukari Tanzania Savegod Moshy, ameeleza kuwa kwa mujibu wa WHO,zaidi ya watu milioni 41 wanaripotiwa kufa kutokana na magonjwa yasiyoambukiza sawa na asilimia 7 ya vifo milioni 57 ulimwenguni kila mwaka.

Kati ya hao,asilimia 37 walikuwa kati ya umri wa miaka 30 hadi 69,ambapo asilimia 85 wakiwa ni kutoka nchi za kipato cha chini na cha kati.

Kwa upande wake Mratibu wa Magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya Shadrack Buswelu, ameeleza kuwa magonjwa hayo mbali na kifo yanaweza kusababisha ulemavu mfano kisukari kinaweza kusababisha mtu kuwa kipofu na kukatwa viungo vya mwili kama vile mguu.

Baadhi ya viungo kushindwa kufanya kazi na kushindwa kufanya mapenzi ipasavyo huku akisisitiza kuwa wagonjwa hao ikiwemo wa kisukari kuzingatia ulaji bora wa chakula ikiwemo vyakula vya wanga.

“Mwili unahitaji nishati ya chakula na wanga lakini hafanye mazoezi ili kuweza kupunguza nishati hiyo na kuendelea kuishi vizuri,”ameeleza Buswelu.

Naye Daktari Waziri Ndonde kutoka shirikisho la vyama vya magonjwa yasiyoambukiza Tanzania,amewaomba Waandishi wa habari kuelimisha jamii juu ya magonjwa yasiyoambukiza.

Dkt.Ndonde, ameeleza kuwa mwangozo wa kuushughulisha mwili na kuepuka tabiabwete(kubweteka),inaonesha kwa namna gani mtu anapaswa kufanya mazoezi kwa usalama.

Ambapo kwa watoto na vijana wa miaka 5-17 kufanya mazoezi kwa dakika 60(saa1) ama zaidi ya uzito wa kati hadi wa ushughulishaji mwili kila siku.

“Siku 3 ndani ya wiki watoto na vijana wanatakiwa wafanye michezo ya kutumia nguvu sana kama vile kukimbia na kucheza mpira,mazoezi ya kuimarisha misuli kama vile kupanda miti, vilima na kusukuma vitu pamoja na mazoezi kuimarisha mifupa kama vile sarakasi na kuruka kamba,”ameeleza

Huku watu wazima miaka 18-64 angalau dakika 150 kwa wiki mazoezi ya uzito wa kati hadi wa juu kama vile kutembea haraka-haraka, siku 2 kwa wiki mazoezi ya kuimarisha Misuli.

Kwa wazee miaka 65 na zaidi angalau dakika 150 kwa wiki mazoezi ya uzito wa kati kama vile kutembea haraka haraka, siku 2 ndani ya wiki mazoezi ya kuimarisha misuli na mazoezi ya kuboresha mwili kuwa na balanzi kama vile kusimama na mguu mmoja.

Aidha Kwa wenye magonjwa sugu na walemavu wanapaswa kufanya mazoezi angalau dakika 150 (kwa mfano, dakika 30 siku 5 kwa wiki) ya uzito wa kati wa mazoezi ya kiaorobikia kwa wiki na ya kuimarisha misuli angalau siku 2 kwa wiki, hii kwa kuhusisha makundi ya misuli mikuu.

Mwenyekiti wa Chama cha ugonjwa wa Kisukari Tanzania Profesa Andrew Swai, akiwasilisha mada katika mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uelewa wa waandishi wa habari kutoka mikoa ya Kanda juu ya namna ya kuripoti habari zinazohusu magonjwa yasiambukiza yaliofanyika jijini Mwanza.
Daktari Waziri Ndonde kutoka shirikisho la vyama vya magonjwa yasiyoambukiza Tanzania Mwenyekiti wa Chama cha ugonjwa wa Kisukari akiwasilisha mada katika mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uelewa wa waandishi wa habari kutoka mikoa ya Kanda juu ya namna ya kuripoti habari zinazohusu magonjwa yasiambukiza yaliofanyika jijini Mwanza.
Mratibu wa Magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya Shadrack Buswelu, akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uelewa wa waandishi wa habari kutoka mikoa ya Kanda juu ya namna ya kuripoti habari zinazohusu magonjwa yasiambukiza yaliofanyika jijini Mwanza.