October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jamii yashauriwa kuenzi vyakula vya asili,miti dawa

Na Penina Malundo,TimesMajira,Online

WITO umetolewa kwa jamii kuhakikisha wana vienzi vyakula vya asili pamoja na miti dawa ya asili ambayo kwa asilimia kubwa inatunza mazingira na kuimarisha afya ya watu.

Akinamama wakiwa kwenye Maonyesho ya Miti Dawa na Vyakula asili katika kuelimisha jamii kujua umuhimu wake katika kuboresha afya na mazingira

Akizungumza jijini Dar es Salaam,Meneja Mradi wa Shirika la Envirocare, Euphrasia Shayo wakati akiongea na waandishi wa habari amesema kuna umuhimu wa kuhamasisha kila rika ikiwemo vijana na watoto kuhakikisha wanashiriki katika kutunza na kuenzi mimea ya miti dawa kwani bado kuna baadhi ya watu wanatumia wanapotaka kujitibu.

Amesema shirika lao la ni miongoni mwa mashirika 52 duniani kote yanayoadhimisha wiki ya kijani ambapo wamekuwa wanatoa elimu kwa Jamii katika masuala mbalimbali hususani utunzaji wa mazingira hususani katika miti na umuhimu wa kula vyakula vya asili.

Shayo amesema katika kuadhimisha maadhimisho hayo ambayo yameanza Julai na kilele kumalizika mwanzoni mwa mwezi huu Oktoba hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wananchi wanajua umuhimu wa utunzaji wa mazingira.

Wanafunzi kutoka shule mbalimbali ya Mkoa wa Tanga wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kupata elimu ya miti dawa na vyakula vya asili jana.

“Shirika lao la Envirocare linashirikiana na Shirika la Swedish Society for Nature Conversation (SSNC) lililopo nchini sweden ambapo wanatoa ufadhili ili kushiriki kuhamasisha masuala ya kijani duniani,ambapo shirika lao katika kuadhimisha siku hiyo waliamua kwenda mkoani Tanga na kutoa elimu juu ya kuenzi na kutunza Miti dawa na utumiaji wa Vyakula vya asili,”amesema Shayo.

Aidha amesema waliweza kufika katika vijiji viwili vya mkoa huo na kufanikiwa kukutana na wananchi mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu hiyo.

“Katika kukutana na wananchi wa vijiji hivyo viwili tuligundua kuwa elimu kuhusu mit dawa inapotea na hata mimea na miti inapotoa kwa sababu utunzaji wake ni mdogo na elimu yake bado haijawafikia watu wengi na kuona kuna umuhimu wa utunzaji wa vitu hivyo ,ambapo kuna haja ya kukusanya kizazi kilichopo na kutoa elimu ili kutambua umuhimu wake,”amesema Shayo.

Amesema shirika lao linahamasisha kuendelea kuenzi na utunzaji wa miti kwa ajili ya kizazi cha baadae katika kuhamasisha umuhimu wa miti hiyo.