November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jamii yahamasishwa kutunza mazingira katika vyanzo vya maji

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online

BODI ya Maji ya Bonde la Wami/ Ruvu ,imesema kuwa katika kuadhimisha siku ya mazingira Duniani juni 5,2021 imeelezea kujikita kuihamasisha jamii kuhusiana na suala zima la Utunzaji wa Mazingira kwenye vyanzo vya Maji.

Mhandisi wa Rasilimali za Maji wa Bodi ya Maji Bonde la Wami / Ruvu, John Kassambili akizungumza wakati wa maonesho ya wiki mazingira.

Pia imesema itaendelea kutoa elimu kwa Makundi mbalimbali ya Wananchi kuhusiana na Matumizi ya Nishati Mbadala ikiwemo Gesi au Nishati banifu.

Akizungumza katika Maonesho ya Wiki ya Mazingira inayofanyika Mjini Dodoma kwenye Viwanja vya Jakaya Kikwete, Mhandisi wa Rasilimali za Maji wa Bodi ya Maji Bonde la Wami / Ruvu, John Kassambili amesema matumizi ya Nishati Mbadala yatasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo mbalimbali vya maji au rasilimali za maji.

“Ukataji wa miti hovyo ni miongoni mwa viashiria hatarishi kwenye suala la utunzaji wa mazingira kwenye vyanzo hivyo vya maji, ambapo matumizi ya nishati mbadala ndio tiba sahihi ya kuendelea kutunza na kuimarisha rasilimali za maji” amesema Mhandisi Kassambili.

Kwa Upande wake, Mmoja wa wananchi waliofika kutembelea maonesho hayo, Mashaka Amrilok ameridhishwa na elimu aliyopatiwa kuhusu Mazingira na Umuhimu wa Matumizi ya Nishati Mbadala katika mizania ya Uhifadhi Endelevu wa vyanzo vya maji.

“ Nimejifunza zaidi kuhusu namna Bodi ya Maji Bonde la Wami / Ruvu inavyoshiriki katika kuangalia vyanzo vya Maji katika Mto Wami lakini pia katika Maeneo mengine ya Mikoa Mbalimbali nchini ikiwemo wanavyofanya Tathmini ya Maji yaliyoko Chini ya Ardhi na Juu ya Ardhi,”alisema

Maonesho ya Wiki ya Mazingira yanaendelea mjini Dodoma na yakitarajia kufikia kilele chake June 5, huku yakibeba Kauli mbiu inayosema Tutumie Nishati Mbadala ili kuongoa Mifumo Ikolojia.