January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jamii yaaswa kupanda miti

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi wananchi wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza wametakiwa kupanda miti huku jumla ya miti 1,000 imepandwa katika eneo la magereza lililopo Kata ya Shibula mtaa wa Ilalila wilayani humo.

Miti iliyopandwa ni pamoja na ya vivuli,mbao na matunda kama michungwa na mipera ambayo imetolewa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).

Akizungumza jana wakati wa zoezi la kupanda miti ikiwa ni moja ya shughuli zinazofanywa na Wilaya hiyo katika kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka 2024,Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Wakili Mariam Msengi amewataka kupanda miti kwa kuzingatia faida nyingi zinapatikana kutokana na uwepo wa miti katika mazingira ya viumbe hai.

” Eneo letu la magereza litanufaika na uwepo wa mandhari nzuri na vivuli punde miti hii itakapokuwa,”.

Kwa upande wake Mkuu wa Magereza Wilaya ya Ilemela Insp.Peter Shoto Kapela ameishukuru TFS kwa kuwapatia miti hiyo huku akiahidi kuilinda na kuleta matokeo chanya yaliyokusudiwa.

Sambamba na tukio la upandaji miti jumla ya mifuko 35 ya saruji imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula kwa ajili ya utengenezwaji wa nguzo kuzungushia mipaka ya eneo la Magereza Ilalila.

Mwakilishi wa Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Fatma Karoli, ameishukuru serikali kwa malipo ya fidia kwa wananchi yaliyofanyika katika eneo hilo la magereza hakika imeondoa migogoro ya ardhi.