Na Grace Gurisha, TimesMajira Online, DSM
JAMHURI imewasilisha pingamizi la awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kupinga maombi yaliyowasilishwa na wadhamini wa Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ya kujiondoa kumdhamini mshtakiwa huyo.
Wadhamini hao ni Ibrahim Ahmed na Robart Katula, ambapo walifikia hatua hiyo kwa madai kwamba wamekosa ushirikiano kutoka kwa Lissu ili kumfikisha mahakamani.
Katika maombi yao, wadhamini wanaomba Mahakama itoe hati ya kumkamata Lissu kwa kuwa wameshindwa kumpata na kumfikisha mahakamani hapo.
Taarifa ya pingamizi ya awali, imewasilishwa mahakamani na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Saimon.
Katika taarifa hiyo, imedai Mahakama hiyo haiwezi kushughulikia jambo hilo na pia haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo na kuyatolea maamuzi, kwa hiyo maombi hayo yatupiliwe mbali.
Maombi hayo, yamekuja leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kwa ajili ya kusikilizwa, ambapo Wakili Wankyo ameomba Mahakama siku 14 ili aweze kujibu maombi hayo kwa njia ya maandishi.
Wankyo amedai kuwa anaomba siku hizo ili aweze kupitia jarada la kesi ya msingi na pia kupitia kesi mbalimbali ambazo zilishatolewa uamuzi.
Baada ya Wankyo kudai hayo, mmoja wa wadhamini hao (Robart) na wao wameomba muda wakuweza kujibu pingamizi hilo, ambapo Hakimu Simba amesema kiutaratibu pingamizi la awali ndiyo linatakiwa kuanza kusikilizwa.
Hakimu Simba amewauliza wadhamini hao kama wanapingamizi na suala la upande wa Jamhuri kuwasilisha majibu yao kwa njia ya maandishi, wamedai kuwa hawana pingamizi.
Amesema upande wa Jamhuri wanatakiwa kuwasilisha majibu hayo Julai 28,2020 na waleta maombi kutakiwa kujibu hoja hizo Agosti 11,2020 na kama kuna majibu ya ziada yatawasilishwa Agosti 18,2020 na kesi itatajwa Agosti 19, mwaka huu, ambapo ndiyo itapangwa tarehe ya uamuzi.
Wankyo amedai katika majibu yake hati ya kiapo kilichowasilishwa mahakamani na waleta maombi hao kuwa Lissu aliruka dhamana tangu siku ambayo alipona na kutoka hospitali.
Amedai kuwa wadhamini hao walikuwa na taarifa za kutosha mahali alipo kwa sababu ilitangazwa na alieleza hivyo hivyo mahakamani, ameeleza kwamba wadhamini wa mshtakiwa namba mbili (Lissu) wanawajibu wa kuhakikisha kwamba anafika mahakamani kwa mujibu wa amri ya Mahakama iliyotolewa Januari 20, mwaka juu na Hakimu Simba.
Kesi ya msingi imeahirishwa hadi Agosti 18, mwaka juu. Mbali na Lissu washtakiwa wengine ni, Wahariri Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.
Katika kesi hiyo washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwamo kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.
Inadaiwa kati ya Januari 12 na 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’
Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.
Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.
Imedaiwa kuwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.
More Stories
TARURA Kilimanjaro yatimiza ahadi ya Rais Samia
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria
Wananchi wakubali yaishe Bangi kubaki historia Tarime