January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jaji aonya mahakimu, watumishi kuomba rushwa

Na Israel Mwaisaka,TimesMajira Online,Sumbawanga

JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, David Mrango amewaonya na kuwataka Mahakimu na watumishi wa mahakama ngazi zote wenye mwenendo usiofaa wa kuomba rushwa na lugha zisizofaa kwa wananchi wajirekebishe.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, David Mrango akikagua gwaride.

Amesisitiza mahakama hiyo,haitasita kuwachukulia hatua kali za kinidhamu na kijinai watakaobainika wanaoendekeza tabia hizo.

Jaji Mrango alitoa karipio hilo katika ufunguzi wa jengo jipya la kisasa la Mahakama ya Mwanzo Laela na Wilaya ya Sumbawanga, katika sherehe zilizofanyika jana katika mji mdogo wa Laela uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa.

“Nitoe rai kwa viongozi wote wahakikishe watumishi wote wa mahakama, wanatoa huduma nzuri zinazoendana na uzuri wa jengo, tujiepushe na lugha zisizofaa kwa wateja wetu ambao ni wananchi na wadau, tujiepushe na vitendo vya rushwa kwani rushwa ni adui wa haki.

“Mahakama haitasita kumchukulia hatua kali za kinidhamu mtumishi yeyote, atakayebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa,” amesisitiza.

Amewaomba Wakuu wa Wilaya za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo kupitia Kamati za Maadili ya Mahakimu kuwaelimisha wananchi kuzitumia kuwasilisha malalamiko ya mienendo isiyofaa kwa baadhi ya mahakimu na watumishi, wanaokiuka maadili wanapotekeleza majukumu yao ya msingi ya utoaji haki.

Amesema ujenzi wa jengo hilo lililogharimu sh.493,026,951 ni matokeo ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa miaka mitano kuanzia 2015/16 hadi 2019/20.

“Hivyo katika mwaka wa fedha 2018/19, Mkoa wa Rukwa ulipata miradi mitatu ya ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo za Msanzi (Kalambo), Mtowisa na Laela (Sumbawanga).

“Uzuri wa jengo hili uambatane na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi na watumishi wa mahakama nasisitiza wanapaswa kubadili mienendo na tabia zinazokiuka miiko na maadili ya kazi na utumishi wa umma, ili watoe huduma kwa ubora unaostahiki,” amesisitiza.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Mohamed Mhando amesema utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 kwamba jengo hilo lilikabidhiwa rasmi Oktoba 2,mwaka huu.