Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Kamati ya viongozi wa dini mbalimbali kuhusu haki za kiuchumi na uadilifu wa uumbaji(ISCEJIC),imetoa ombi kwa serikali kuchukulia suala la afya kama uwekezaji.
Ambapo hali hiyo itasaidia suala zima la mpango wa bima ya afya kwa wote kwani afya ni moja ya mambo muhimu ya maendeleo ya binadamu na uchumi wa taifa.
Akizungumza katika mkutano wa uongezaji uwezo na taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu mapendekezo ya viongozi wa dini Tanzania kuhusu umuhimu wa kupitishwa kwa sheria ya bima ya afya kwa wote nchini uliofanyika mkoani Mwanza, Mwenyekiti Mwenza wa ISCEJIC Sheikh Khamis Mataka, amesema dini zao siku zote zinaamini kwamba jamii yenye afya njema ni jamii yenye imani thabiti.
Sheikh Mataka, amesema kuanzia mwaka 2017, waliojikita katika kampeni ya hifadhi ya jamii hasa katika afya ambayo ilitanguliwa na utafiti ulioitwa ‘Make it possible’ yani tufanye afya kwa wote kuwa kitu kinachowezekana.
“Kutokana na matokeo ya utafiti huu, viongozi wa dini walitoa mapendekezo mbalimbali ikiwemo bajeti ya kugharamia afya isichukuliwe kama gharama bali ichukuliwe kama uwekezaji katika maendeleo ya mwanadamu ambayo ndio msingi wa kila kitu,” amesema Sheikh Mataka.
Amesema wanakumbana na kesi za waumini wanahitaji kipimo cha MRI ambacho ni shilingi 500,000,familia imemchangia msikitini ameenda kuomba wamemchangia amekusanya fedha kapata laki tatu na kile kipimo kinahitaji fedha zaidi.
Hali ambayo inakwamisha mtu huyo ambaye hana uwezo kukipata kipimo hicho,hivyo jambo la kuwa na bima ya afya ya matibabu kwa wote ni muhimu.
“Muumini mwenye afya ni bora kuliko muumini dhaifu,kwani ana nafasi ya kuchangia maendeleo ya nchi na yake binafsi na familia yake na dhaifu ni mzigo kwa jamii kwaio tuboreshe haya mambo ya afya,ili suala la bima ya afya kwa wote litimie na sheria husika ije haraka iwezekanavyo,”amesema.
Sanjari na hayo amesema serikali kwa kushirikiana na wadau wengine ihakikishe watanzania wanaelewa na wanahimizwa kujiunga na bima ya afya ilioboreshwa pamoja kuongeza wigo wa walipa kodi na kutenga kodi maalum kwa ajili ya kugharamia afya.
Pia amesema, serikali iboreshe kitita cha huduma ya bima ya afya kiwiane na malipo na bei ya soko ili kuondoa changamoto katika utoaji wa huduma na kuwa na maeneo maalum ya kodi ambayo itapelekwa katika kuboresha sekta ya afya.
Mwenyekiti wa ISCEJIC Askofu Nelson Kisare amesema,wakati serikali inaandaa na kuleta muswada mpya wa bima ya afya kwa wote,wanapendekeza serikali ijikite kwa nguvu sana katika kuelimisha jamii kuhusu dhana ya bima ili wajiunge wengi zaidi.
Ambao wataongeza wigo mpana wa kuwa na mfumo imara wa bima pia serikali itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kuratibu na kuelimisha watu na shughuli ya kuandikisha watu katika bima hiyo ya afya kwa wote huku waandishi wa habari waelimisha jamiii kuhusiana na suala zima la bima.
Pia amesema, serikali lazima iweke kipaumbele endelevu cha kiwango cha fedha kitakachokuwa kinachangiwa na serikali katika kuendesha bima ya afya kwa wote ambayo mwananchi atachangia na serikali itachangia.
“Suala la bima ya afya hatutegemei serikali kwa asilimia miamoja kwani kuna Watanzania ambao wanauwezo wa kuchangia,bima ya afya kwa wote ikianza uhitaji utaongezeka hivyo wataalamu pia wanahitajika kuongezwa,” amesema Askofu Kisare.
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Hassan Kabeke, amesema wito kwa jamii ni vizuri wakasikiliza viongozi wao wa dini kwani ukiwa hauna bima ukiuguza au kuumwa ni mzigo mkubwa.
“Watanzania mpango wa bima unapaswa kuungwa mkono kwani hakuna jambo kubwa kama afya huku serikali walichukulie jambo hilo kwa haraka,”.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza Edwin Soko amesema ni wajibu wao waandishi wa habari kuelimisha jamii hivyo watatangaza na kuhabarisha umma ili iweze kufahamu juu ya suala hilo la bima ya afya kwa wote.
Mratibu wa Kamati ya Amani Mkoa wa Mwanza, Sheikh Twaha Bakari,alimuomba Rais kutumia tozo za mihamala ya huduma za kifedha za mitandao ya simu angalau za miezi miwili zitumike katika suala zima la bima kwa wote kwa watanzania.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa