Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online,Tanga
WAZIRI wa Mambo ya Nje ya Nchi wa nchini Ireland, Neale Richmond, amesema nchi hiyo imeridhishwa na mradi wa mafunzo kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii na itaendelea kufadhili mpango huo kusaidia kukabiliana na magonjwa na kuokoa vifo vya wajawazito na watoto.
Waziri huyo amebainisha hayo katika ziara yake jijini Tanga,yenye lengo la kuona maendeleo ya mradi wa huduma ya afya ngazi ya jamii unaolenga kukabiliana na magonjwa mbalimbali.

Akizungumza mara baada ya kufika katika kituo cha afya cha Mikanjuni,Waziri huyo amesema kwamba ni wasaa mzuri kusikia kutoka kwa wahudumu wanaofanya kazi ya kutoa huduma za afya ngazi ya jamii na wale wanaofanya kazi kwenye vituo vya kutolea huduma na wale ambao wanasaidia kufanya maisha ya jamii kuwa mazuri katika Mkoa wa Tanga.
“Tuna furaha ya kuendelea kufadhili mradi huu na tutaendeklea kushirikiana na Serikali ya Tanzania na taasisi nyingine kuona ufadhili unakuwa endelevu,”amesema Waziri huyo.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamini Mkapa Foundation,Dkt.Helen Senkoro, amesema kwamba programu hiyo wanayoitekeleza kwa jamii ni ya kitaifa na nchi ya Ireland,imeahidi kuendelea kuunga mkono mikakati ya kitaifa kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine ikiwemo taasisi hii.
Dkt.Senkoro amesema kwamba sehemu ambazo wamekuwa wakiwawezesha ni kujenga mifumo endelevu ya kutoa huduma za afya ikiwemo upatikanaji wa watumishi ambapo kwa kushirikiana na taasisi hiyo wameweza kuajiri watumishi 450 sehemu mbalimbali nchini ikiwemo Bara na Visiwani.
“Ireland ni mmoja ya mdau ambaye amekuwa anatuwezesha kama taasisi na tumekuwa tukishirikiana nao kwa zaidi ya miaka 10,na fedha ambazo wametoa ni takribani bilioni 21 kwa miaka hiyo, katika kuimarisha huduma za afya,”amebainisha Dkt.Senkoro.
Naye John Sagaika Mratibu wa Elimu ya Afya kwa umma ngazi ya Mkoa, amesema wao kama sekta ya afya Mkoa Tanga wanatoa shukrani kwa ubalozi wa Ireland kwa kufanikisha kupeleka mafunzo kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii 440 ambao wamepata mafunzo kwa miezi 6.
Ambapo miezi mitatu darasani na miezi mitatu kwa vitendo jambo ambalo limekwenda kuleta mtazamo chanya kwa jamii ikiwemo kiubua wagonjwa wapya ngazi ya jamii.

Kwa upande wake Muhudumu wa afya ngazi ya jamii Najma Twalibu,amesema kwamba mradi huo umeweza kuwasaidia kwa kiwango kikubwa ikiwemo kupunguza idadi ya watu wanaoishi kwa matumaini waliopoteza muelekeo kwenye vituo vya afya.
Ambapo kwa huduma wanazotoa za nyumba kwa nyumba wameweza kuwapata na kuwarudisha katika vituo vyao na kuendelea kupata huduma.
Hiyo ni sehemu ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi, nchini Ireland ya kutembelea miji 90 duniani ambayo ina miradi ya afya inayotekelezwa kwa ufadhili wa nchi hiyo.

More Stories
MSIGWA:Mfumo wa usajili waandishi wa habari kidijitali upo mbioni kukamilika
Kongani ya Viwanda ya Sino _Tan kutoa ajira laki moja
Waandishi wa habari kutambulika kidijitali