March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

INEC yawahakikishia watanzania kusimamia, Uchaguzi Mkuu kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni na Taratibu

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

TUME huru ya Taifa ya uchaguzi (INEC) imewahakikishia Watanzania kusimamia
Uchaguzi Mkuu kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni na Taratibu mbalimbali zinazosimamia uendeshaji wa uchaguzi, lengo ikiwa uchaguzi unakuwa huru, uwazi, haki na wa kuaminika kwa kuweka mazingira sawa ya ushindani kwa wagombea na vyama vyote vya siasa vitakavyoshirki.

Akizungumza leo jijini Dar es salaam kwenye Mkutano Maalum wa Wawakilishi wa Taasisi na Asasi za Kiraia,Mwenyekiti wa Tume huru ya Taifa ya uchaguzi Jaji (Rufani) Jacobs Mwambegele
amesema
katika kipindi cha uchaguzi Tume imejipanga kufanya kazi kwa karibu na Taasisi na Asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura.

Amesema Wawakilishi hao waliopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na maelekezo ya Tume wakati wote wa utekelezaji wa zoezi hilo la kutoa elimu ya mpiga kura.

Amesema hadi sasa Tume imefanya maandalizi mbalimbali ya Uchaguzi Mkuu na ili zoezi hilo liweze kufanikiwa kwa kiwango kikubwa linategemea ushirikiano wa Wawakilishi wa Taasisi na Asasi za Kiraia, katika kuwaelimisha Wananchi juu ya umuhimu wa zoezi hili.

“Tume inaamini kuwa mkishirikishwa vyema na mkapata uelewa wa kutosha kuhusu mchakato wa uchaguzi, itakuwa rahisi pia, kuwaelimisha wananchi.

“Niwaombe msichoke kuwasisitiza na kuwahimiza wadau na wananchi kwa ujumla kuzingatia Sheria za Uchaguzi, Kanuni na Maelekezo ya Tume,Tume nayo kwa upande wake itaendelea kuzingatia Sheria za Uchaguzi na Kanuni katika michakato yote ya uchaguzi,”amesema.

Jaji Mwambegele amesema kupitia mkutano huo wa wawakilishi wa Taasisi na Asasi za Kiraia wanaimani wataendelea kupata ushirikiano mkubwa zaidi kutoka kwao na kutumia nafasi zaon kwa jamii kuwafikishia taarifa sahihi na kwa wakati.

Amesema miongoni mwa taarifa ambazo wawakilishi hao na Asasi za Kiraia zinapaswa kufikishwa kwa wananchi ni pamoja na hatua iliyofikiwa sasa katika maandalizi ya uchaguzi Mkuu 2025,ikiwa ni pamoja na kuwahasisha wananchi waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura,wajitokeze kwa wingi kupiga kura kuwachagua viongozi wanaowataka.

“Tume inashukuru kwa michango yenu namna ambavyo mmekuwa mkishirikiana nasi kwa kuwafikishia taarifa wadau ambao ni wanachama wa majukwaa yenu na michakato mbalimbali ya uchaguzi.

“Tume inawatambua wawakilishi wa taasisi na asasi za kiraia kwa namna mbili,ikiwemo kama daraja linalounganisha Tume na wadau kwa njia ya elimu na kama moja ya wadau muhimu wa uchaguzi, kutokana na ukweli huo Tume imeona umuhimu wa kufanya kikao cha pamoja Ili kupeana taarifa na kufahamishana kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu huu,”amesema Jaji Mwambegele

Aidha Jaji Mwambegele amesema wakishirikishwa vyema na kupatiwa uelewa wa kutosha wawakilishi wa taasisi na asasi za kiraia kuhusu mchakato wa uchaguzi, itakuwa rahisi kwao kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kupitia majukwaa yao kuweze kushiriki kikamilifu uchaguzi mkuu 2025.

“Dhamira hiyo ndiyo iliyoisukuma Tume kuandaa kikao cha pamoja ili kupeana taarifa na kuhamasishana kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu mwaka huu,”amesema.

Amesema julai 26, 2025 ,Tume huru ya Taifaya uchaguzi kwa Mamlaka iliyopewa chini ya masharti ya ibara 41(4) ya katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na kifungu cha 49(1) (a)na 68(1)vya Sheria ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024 lilitangaza ratiba ya uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge katika Jamhuri ya Muungano na Madiwani kwa Tanzania bara 2025.

:Tume ina matumaini makubwa ya kufanikisha uchaguzi huu kwa kutegemea ushiriki wenu katika hatua zote zilizosalia Hadi kumfikia siku ya uchaguzi. Imani hii inatokana na ushirikiano mlioonesha hususani wakati wa uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura,”amesisitiza