Na Allan Kitwe, Timesmajira Online-Tabora
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC),imesema itavitendea haki sawa vyama vya siasa vitakavyoshiriki uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.
Hayo yamebainishwa na Kamishna wa Tume hiyo,Magdalena Rwebangira,wakati akifungua mafunzo ya siku 3 kwa waratibu,wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Jimbo kutoka Mikoa ya Tabora na Kigoma yanayofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agoustino(SAUT),Mjini Tabora.

Amesema kuwa Tume imeleta mafunzo hayo ili kuwaandaa vyema,waratibu, wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi huo ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Pia amesisitiza kuwa Tume imejipanga vizuri ili kuhakikisha taratibu zote za kikatiba na kisheria zinazingatiwa na kufuatwa, na wote waliopewa dhamana ya kusimamia uchaguzi huo ili kuhakikisha unakuwa na ufanisi.
Hata hivyo amewataka washiriki wa mafunzo hayo,kusoma kwa umakini katiba, sheria, kanuni, miongozo na melekezo yote yanayotolewa na Tume,ili kuwarahisishia utekelezaji jukumu hilo na kuepusha malalamiko na vurugu wakati wa mchakato wa uchaguzi.
‘Shirikisheni vyama vya siasa vyote vitakavyoshiriki uchaguzi katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi huo, hakikisheni kanuni, taratibu, sheria, miongozo na maelekezo yote ya tume yanazingatiwa ili kuepusha malalamiko,” amesema.
Aidha amewataka kushirikisha wadau wanaostahili katika maeneo ambayo Tume imeelekeza na kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema na kubaini mahitaji maalumu vya vituo husika ili uchaguzi ufanyike kwa amani na utulivu.
Kuhusu ajira za watendaji wa vituo vya kupigia kura, Kamishna amewataka kutoingiza watu wasio na sifa kwa kigezo cha undugu au jamaa bali wazingatie weledi, uzalendo, uadilifu na uchapa kazi.

Amewataka kukagua na kuhakiki vifaa vya uchaguzi wanavyopokea na kuvisambaza katika maeneo husika kwa wakati, kutoa taarifa wakati wa kuapisha mawakala na kuhakikisha vyama vinapewa orodha ya vituo vya kupigia kura ili viweze kupanga mawakala wao vizuri.
Akiongea kwa niaba ya Washiriki wenzake, Msimamizi wa Uchaguzi wa Manispaa ya Tabora,Paschal Matagi,ameeleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu na yatawasaidia kufanikisha jukumu hilo kwa ufanisi.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako