November 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Indonesia yawavutia wengi maonesho ya vyakula vya asili Dar

Na Bakari Lulela,TimesMajira Online

WAKAZI wa Mkoa wa Dar es Salaam wamejitokeza kwa wingi katika maonesho ya kimataifa ya vyakula vya asili kutoka nchi mbalimbali duniani yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam

Baadhi ya wananachi waliojitokeza kwenye maonesho ya kimataifa ya vyakula asili wakipata maelezo ya upikaji wa vyakula vya asili katika viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam,

Akizungumza katika ufunguzi wa maonyesho ya kwanza ya kimataifa ya vyakula hivyo yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam mgeni rasmi katika maonesho hayo Kaimu Balozi kutoka Ubalozi wa Indonesia nchini Wahono Yulianto amesema nchi Indonesia hutumia viungo mbalimbali katika uandaaji wa vyakula hivyo ambapo pia hupatikana katika nchi ya Tanzania ikiwemo mihogo,ndizi, viazi mviringo na karanga.

Amesema maonyesho hayo yanawapa fursa Watanzania kubadilishana uzoefu na washiriki kutoka nchi nyingine.

Kaimu Balozi kutoka Ubalozi wa Indonesia nchini Wahono Yulianto (Wa kwanza kulia) akipata maelezo ya namna ya upikaji wa vyakula cha asili

“Lengo la maonyesho haya ni kujenga mahusiano pamoja na kuwaonyesha watanzania aina mbalimbali ya vyakula vinavyopatikana nchini Indonesia kiasi ambacho hupikwa kwa kutumia viungo ambavyo pia hupatikana Tanzania,” amesema Yulianto

Aidha Kaimu huyo amesema kwa kuongeza kwamba maonyesho hayo yanaweza kutumika kama njia ya kufahamiana kwa kujenga mahusiano mema baina ya nchi Indonesia na Tanzania sambamba na taasisi zingine zilizoshiriki maonyesho hayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Masuala ya Utamaduni kutoka Ubalozi wa Indonesia Joan Radina Setiawan alieleza ushiriki wao kwenye maonyesho ni pamoja na utoji wa mafunzo ya mapishi kwa makundi mbalimbali ya wanajamii kwa kudai kwamba ni sehemu ya utamaduni katika nchi yao.

Hata hivyo Mkuu huyo amefafanua kuwa upikaji wa chakula kizuri unatokana na ubunifu aliokuwa nao muandaaji ambaye hutumia maarifa kwa kukifanya kinakuwa na radha bora yenye kumvutia mlaji.

Naye muandaaji wa Maonyesho kutoka taasisi ya Sapota hapa nchini Ally Mchume amesema maonyesho hayo alikuwa ya siku 3 yamezishirikisha zaidi ya nchi 15 Duniani zikiwemo China,Tanzania,Indonesia, Mexico,Vietnam na Ufaransa.

“Maonyesho haya yanalengo la kujenga mahusiano mema ya kitamaduni kati ya nchi hizi ambapo Tanzania kama mwenyeji imeonesha umadhubuti katika uandaaji wa vyakula bora vya kitamaduni,” amesema Mchume.