June 12, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ILO:Uhamiaji ukisimamiwa vizuri ni fursa ya Maendeleo

Na.Mwandishi wetu,Timesmajira

Mshauri Mkuu wa Kiufundi kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO), Aida Awel, amesema kuwa uhamiaji ni sehemu ya uhalisia wa maisha ya jamii za kisasa na unaweza kuwa fursa kubwa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii iwapo utasimamiwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.

Awel alitoa kauli hiyo juzi jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kikao maalum kilichoandaliwa na ILO kujadili masuala ya wahamiaji wafanyakazi nchini Tanzania na katika Ukanda wa Pembe ya Afrika Mashariki na Afrika (EHoA).

Akizungumza katika kikao hicho, amesema usimamizi mzuri wa masuala ya uhamiaji unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya nchi za kikanda ili kuhakikisha wafanyakazi wahamiaji wanapata mazingira salama ya kufanya kazi huku haki zao zikilindwa ipasavyo.

Ameeleza kuwa uhamiaji salama na wenye mpangilio mzuri unaweza kuleta manufaa makubwa kwa nchi za asili za wahamiaji, hususan pale wafanyakazi wanapopata ajira zenye staha katika nchi wanazokwenda na kuwa na uwezo wa kutuma fedha kwa familia zao bila kukumbana na ukiukwaji wa haki za binadamu.

“Uhamiaji ni uhalisia wa maisha na pia ni fursa iwapo utasimamiwa vizuri. Utawala bora wa masuala ya uhamiaji husaidia kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi wahamiaji pamoja na wananchi wa nchi zetu,”amesema Awel.

Aidha, amebainisha kuwa mafanikio katika usimamizi wa uhamiaji yanategemea uwezo wa nchi kuimarisha mifumo mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo kulinda haki za binadamu, kuandaa sera na takwimu sahihi, kuongeza uelewa kwa umma kuhusu masuala ya uhamiaji na kuzijengea uwezo taasisi zinazohusika na sekta hiyo.

Kwa mujibu wake, hatua hizo zitasaidia kuondoa mtazamo hasi unaouona uhamiaji kama tishio na badala yake kuutambua kama nyenzo muhimu inayoweza kuchangia maendeleo ya kiuchumi, kijamii na ustawi wa wananchi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Awel amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya nchi mbalimbali ili kuhakikisha kunakuwepo na mifumo madhubuti ya kusimamia uhamiaji wa wafanyakazi kwa manufaa ya wahamiaji wenyewe, familia zao na uchumi wa nchi husika.

Wadau wa sekta ya kazi na uhamiaji wanaamini kuwa ushirikiano wa kikanda pamoja na sera rafiki kwa wafanyakazi wahamiaji ni miongoni mwa nyenzo muhimu zitakazochochea uhamiaji salama, wenye tija na unaochangia maendeleo endelevu katika ukanda huo.