May 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ilemela yatenga milioni 920 kwa ajili ya mikopo ya vikundi

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online – Mwanza

Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza imetenga kiasi cha shilingi milioni 920 kwa ajili ya mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi 60 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Kwa mujibu wa Ofisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa Asasi za Kiraia wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela , Yusuph Omollo,amesema, wanawake watapata asilimia 4 na vijana asilimia 4 huku watu wenye ulemavu asilimia 2 ya kiasi hicho.

Akizungumza Mei 12, 2025 na Timesmajira Online kwenye kongamano la Maendeleo ya Jamii lililofanyika Uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela, Omollo,amesema lengo la kongamano hilo ni kutoa elimu kuhusu namna ya kuomba mikopo kupitia mfumo wa “Wezesha Portal”,kwani mtaani kuna maneno ambayo siyo sahihi yanayowadang’anya wananchi na kujikuta wakiliwa fedha zao.

“Kwa sasa tumeisha toa awamu ya kwanza ya mikopo. Tunategemea kufanikisha awamu ya pili kabla ya Juni 15, 2025, endapo hakutatokea changamoto yoyote,rai yangu kwa watakao pata mikopo wairejeshe kwani siyo msaada,”amesema Omollo.

Ameeleza kuwa,kabla ya vikundi kupewa mikopo, hupatiwa mafunzo ya ujasiriamali na uendeshaji wa biashara. Pia Maofisa Maendeleo ya Jamii wa kata watakuwa wakitoa semina za mara kwa mara kwa vikundi vilivyopewa mikopo au vinavyotarajia kukopa ili viweze kuendesha biashara na kurejesha mkopo bila usumbufu.

Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Sangabuye, Paskazia Muyanja, amewahimiza wanawake kuchangamkia fursa ya mikopo ya Halmashauri,ambapo ameeleza kuwa lengo ni kusaidia wanawake kujikwamua kiuchumi na kuepuka mikopo ya riba kubwa maarufu “kausha damu”.

“Tunawahimiza wawekeze katika miradi ya uzalishaji badala ya kugawana fedha. Mikopo hii haina riba na inatoa muda wa miezi mitatu ya kujipanga kabla ya kuanza kurejesha,”amesema Paskazia.

Naye Getruda Itoba kutoka kikundi cha Buyegu, aliwahamasisha wanawake wenzake kujiunga na kutumia fursa hiyo kuanzisha miradi midogo ya kiuchumi ili kujikwamua na kuondokana na utegemezi.