*Ikiwa ni mara ya tano mfululizo,mshikamano ndio siri ya mafanikio
*Asilimia 71 ya hoja zafungwa
*Kukosekana kwa mikakati thabiti sababu ya baadhi ya hoja kutokufungwa
Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online – Mwanza
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza imepata hati safi ya ukaguzi wa hesabu kwa mwaka wa fedha 2023/2024, ikiwa ni mara ya tano mfululizo tangu mwaka wa fedha 2019/2020.
Hatua hiyo inaifanya halmashauri hiyo kuwa miongoni mwa taasisi za serikali zinazotambulika kwa uwajibikaji na usimamizi thabiti wa rasilimali za umma.

Hayo yamebainishwa katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo,kilichofanyika Juni 17,2025, cha kupokea na kujadili taarifa ya hoja zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na utekelezaji wake.
Akiwasilisha taarifa ya hoja zilizojitokeza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,Mweka Hazina wa Manispaa ya Ilemela, Mariam Mshana,amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024,halmashauri ilikutwa na hoja 42, ambapo kufikia sasa hoja 30 zimefungwa na 12 zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, hii ni sawa na asilimia 71 ya hoja kufungwa.
“Halmashauri yetu imeendelea kupata hati safi kwa miaka mitano mfululizo kwa sababu ya mshikamano miongoni mwa Madiwani, ofisi ya Mkuu wa Wilaya, ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na timu ya wataalamu katika kutekeleza majukumu kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu,”amesema Mariam.
Awali Mkaguzi wa Mkuu wa nje wa Mkoa wa Mwanza,CPA. Richson Ringo,amesema,katika mwaka 2023/2024 Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ilipata hati safi.Huku kwa miaka ya nyuma Halmashauri hiyo ilikuwa na mapendekezo 16,ambapo hoja 12 zilihakikiwa na kufungwa na hoja nne bado zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Ringo amesema,sababu ya mapendekezo au hoja,zilizosalia kutokufungwa inatokana na kukosekana kwa mikakati thabiti na ya dhati kwa watekelezaji,pamoja na wakuu wa idara wanaohusika na hoja hizo kutoshirikishwa ipasavyo huku majibu ya menejimenti yanakosa vielelezo na ushahidi wa kutosha ili kuwezesha kufungwa kwa hoja hizo.

Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula,”Kuna hoja nne ambazo bado hazijafungwa, mojawapo ikiwa ni ya mwaka 2015/2016,ambayo Halmashauri ya Jiji la Mwanza iliuza eneo la Halmashauri ya Ilemela ambayo kimsingi ilianza mwaka 2012, na mgawanyo wa mali ulikuwa tayari.Mbaya kila mwaka hoja inajirudia ,naomba Mkuu wa Mkoa utusaidie kuona Ilemela tunapata haki yetu na hoja hii inafungwa,”.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Ummy Wayayu,amesema hoja ya muda mrefu ambayo haijafungwa ni ya uuzwaji wa kiwanja eneo la Gana ambalo lipo katika Halmashauri hii ulifanywa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza.Hivyo kupitia ofisi ya Mkuu wa Mkoa wanaendelea kufanyia kazi suala hilo hili kuona namna ya kulimaliza.
“Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda,amesema suala hili baada ya kukamilika kwa hoja hizi, ataitisha menejimenti zetu ili kwa pamoja tuone tunaendaje kumaliza hoja hiyo.Kwa sababu utekelezaji wa hoja hiyo kwa mujibu wa Mkaguzi wa nje,ni kwamba Halmashauri ya Jiji irejeshe fedha hizo za uuzwaji wa kiwanja kwa Manispaa ya Ilemela,”amesema Wayayu.
Wayayu,amesema,hoja nyingine ambayo ilikuwa ya muda mrefu, ina husiana na uuzwaji wa viwanja.”Tulikuwa na mradi wa uuzwaji wa viwanja ambao ulikuwa ni zaidi ya bilioni 1,watu walinunua viwanja hivyo lakini hawajakamilisha malipo.Hivyo mwaka huu tumefuatilia na tulichojipanga na wataalamu wangu,wapitie viwanja vilivyosalia kimoja baada ya kingine,nitatoa matangazo ya kuuza tena viwanja hivyo na tutawakabidhi wanunuzi wapya,”
“Kwa wale walionunua awali tutaona nini cha kufanya,kwani kwa mujibu wa sheria wanatakiwa kukamilisha malipo ndani ya siku 90, na sasa hivi ukiangalia ni zaidi ya miaka mitatu tangu kuanza mradi huo,”.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Said Mtanda,ameitaka Halmashauri hiyo kuhakikisha haizalushi hoja mpya za ukaguzi kwa kuzijibu kwa wakati,zifungwe na watekeleze maoni yanayotolewa na CAG, pamoja na kushirikiana naye ili kuendelea kuzipatia majibu hoja hizo.Huku akisisitiza ushirikishwaji wa idara zote wakati wa mujibu hoja zinapojitokeza.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi