November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ilemela yalenga kuimarisha miundombinu mwaka wa fedha 2023/2024

Na Judith Ferdinand,Timesmajira Online, Mwanza
Ikiwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 unaelekea ukingoni Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela inatarajia kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2023/2024.


Ambapo kwa mwaka huo mpya wa fedha wa 2023/2024 Ilemela inatarajia kutekeleza miradi mkakati hiyo kwa lengo la kuimarisha na kuboresha miundombinu na kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.


Hayo yamebainishwa katika taarifa iliyotolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Juni 19,2023 ambayo imeanisha miradi mikakati hiyo ambayo imelenga kuimarisha na kuboresha miundombinu ya miradi mikakati hiyo.


Taarifa hiyo imetaja miongoni mwa miradi mikakati ambayo halmashauri inalenda kuitekeleza ni pamoja na ujenzi wa soko kuu la kisasa Kirumba pamoja na barabara zinazozunguka soko kupitia program ya TACTIC kwa ushirikiano na Benki ya Dunia.


Mradi mwingine ni uboreshaji wa uwanja wa Furahisha kwa ajili ya matumizi ya biashara na shughuli za kijamii ili kuweka mazingira mazuri ya maeneo ya burudani kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya.
Pia mradi mwingine ni ujenzi wa barabara za kiwango cha lami za Buswelu-Busenga-Cocacola,Mbogamboga-Nyamadoke-Nyamhongolo,Pasiansi-Lumala-Kiseke na Kahama-Ilaila-Kabusungu kupitia program TACTIC ili kuongeza uwekezaji na idadi ya biashara.


Mbali na hiyo mradi mwingine ni uboreshaji wa soko la kimataifa la mazao ya samaki Mwaloni Kirumba kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya.