December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ilemela yakusanya zaidi ya bilioni 12

Judith Ferdinand, Timesmajira online, Mwanza

Hadi kufikia Machi mwaka huu, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imefanikiwa kukusanya zaidi ya bilioni 12.1, sawa na asilimia 90 ya makisio ya bajeti ya mwaka 2022/2023.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary,wakati akiwasilisha taarifa yake katika kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo kwa kipindi cha robo ya tatu Januari-Machi mwaka wa fedha wa 2022/23, kilichofanyika Mei, 15,mwaka huu.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary.

Mhandisi Modest, ameeleza kuwa mapato hayo ni ya ndani huku mapato halisi ni zaidi ya bilioni bilioni 11.9, sawa na asilimia 92 ya bajeti.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa kwa robo ya tatu hiyo kiasi cha zaidi ya bilioni 1.5,zilielekezwa kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo katika kata.

Ambapo kwenye sekta ya elimu Mhandisi Modest, ameeleza kuwa elimu msingi wamepeleka zaidi ya milioni 131 kati ya hizo milioni 29.1,kwa ajili ya utengenezaji wa madawati katika shule ya msingi Kahama,zaidi ya laki 4,kwa ajili ya malipo ya mafundi katika ujenzi wa bweni la watoto wenye uhitaji Maalum shule ya msingi Buswelu.

Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, waliohudhuria kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo kwa kipindi cha robo ya tatu Januari-Machi mwaka wa fedha wa 2022/23, kilichofanyika Mei, 15,mwaka huu.

Huku kiasi cha milioni 16 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mwalimu shule ya msingi Nyamh’ongolo, milioni 20.4 kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba 2 vya madarasa shule ya msingi Buhongwa.

Zaidi ya laki 5,kwa ajili ya ukarabati wa vyoo shule ya msingi Ihalalo, zaidi ya milioni 28.2, ukamilishaji wa vyumba vya madarasa 7 na ofisi 2 shule ya msingi Shibula,milioni 15, ujenzi wa matundu 10 ya vyoo katika shule ya msingi Shibula pamoja na milioni 21.2 kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba vya madarasa shule ya msingi Buyombe.

Kwa upande wa elimu sekondari wamepeleka milioni 30 kwa ajili ya ukamilishaji wa maabara ya Sayansi pamoja na choo shule ya sekondari Buzuruga.Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa katika sekta ya afya wametoa zaidi ya milioni 74.4 kati ya hizo zaidi ya milioni 8.8 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la RCH zahanati ya Nyamh’ongolo.

Huku zaidi ya milioni 12 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya ujenzi pamoja na malipo ya fundi katika hospitali ya Wilaya,milioni 39 ukamilishaji wa wodi ya kina mama katika kituo cha afya Buzuruga na milioni 23.6 ujenzi wa jengo la RCH zahanati mpya ya Kawekamo.

Vilevile ameeleza katika sekta ya utawala wamepeleka zaidi ya milioni 245.5, biashara,viwanda na uwekezaji milioni 85.8, miundombinu milioni 23.6, mipango Miji milioni 780.5 huku mifugo na uvuvi zaidi ya milioni 14.1.

Baadhi ya Madiwani wakichangia taarifa hiyo akiwemo Diwani wa Kata ya Kiseke Ramadhani Mwevi,wamempongeza Mkurugenzi huyo kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato na kufanikiwa kufikisha asilimia 90 ya makisio ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/23.