December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ilemela yafanikiwa kukusanya asilimia 95 ya makisio ya bajeti 2023/24

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imefanikiwa kukusanya kiasi cha bilioni 13.6 sawa na asilimia 95 ya makisio ya bajeti ya mapato ya ndani.

Fedha hiyo imekusanya hadi kufikia Juni mwaka huu,ambapo Halmashauri hiyo ilipanga kukusanya kiasi cha bilioni zaidi ya bilioni 14.

Hayo yamebainishwa Agosti 2,2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Ummy Wayayu,wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi na uwajibikaji wa Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24, kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya nne ya mwaka huo wa fedha, kilichofanyika ukumbi wa Halmashauri hiyo.

“Halmashauri ilipanga kukusanya na kutumia kiasi cha bilioni 70.4, kati ya fedha hizo bilioni 43.5 ni mishahara,mapato ya ndani ni zaidi ya bilioni 14 na matumizi mengine ni bilioni 1 huku fedha za miradi ya maendeleo kutoka kwa wafadhili na ruzuku ni bilioni 11,”.

Katika sekta ya utawala na rasilimali watu Halmashauri hiyo ina jumla ya watumishi 3511 mahitaji ni 4409 upungufu 898, hususani katika sekta za ujenzi,walimu wa masomo ya Sayansi, wataalamu wa sekta ya afya na Watendaji wa mitaa huku katika mwaka huo watumishi wapya 13 wameajiriwa.

Fedha ilioyolewa ya elimu bila malipo kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Juni 2024 ni milioni 905.5 huku sekondari bilioni 3.8 zilitolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu ya sekondari katika kipindi hicho.

Kwa upande wake Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Manusura Sadick,ameeleza kuwa amekuwa akisimamia mapato ya ndani na fedha kutoka serikali kuu vizuri pamoja na kushirikiana na Madiwani hao kutatua changamoto hasa zinazogusa Kata zao katika miradi mbalimbali ikiwemo afya.

“Katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2023/24 kila Kata imepelekewa fedha,hakuna Kata iliyopokea chini ya milioni 60, fedha zinazotokana na mapato ya ndani, najitahidi kupitia mapato ya ndani ile miradi ilioanzishwa na wananchi inakamilika,”.

Hata hivyo ameeleza kuwa katika awamu ilioanza Julai Mosi,2024 wanampango wa kuidhinisha zaidi ya bilioni 3.5, na wameisha pitisha fedha za awali zaidi ya milioni 300 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali vya ujenzi wa barabara.

“Agosti 16, mwaka huu tunakwenda kupitisha fedha nyingine zaidi ya bilioni 3.2, kwa ajili ya Halmashauri kununua magreda yake,malori ili kumuunga mkono Rais katika ujenzi wa barabara zilizoharibika,”ameeleza Manusura.

Naye Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula amewahimiza Madiwani wa Halmashauri hiyo kuendelea kusimamia miradi na suala zima la matumizi ya fedha.