November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

IGUWASA yaomba mabadiliko ya bei huduma za maji

Na Lubango Mleka, TimesMajiraOnline Igunga.

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora (IGUWASA) imetoa ombi la mapendekezo ya mabadiliko ya bei na ada za huduma ya maji kwa wananchi wilayani hapa.

Maombi hayo yamewasilishwa kwenye kikao maalumu cha utoaji wa maoni kutoka kwa wananchi juu ya maombi hayo ya IGUWASA kilichoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kilichofanyika katika ukumbi wa Maxwell mjini hapa, ambapo mgeni rasmi ni Mkuu wa Wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo.

Akitoa maelezo ya utangulizi juu ya EWURA, Meneja EWURA kanda ya Kati Hawa Shani Lweno amesema kuwa, kwa mujibu wa sheria ya EWURA Sura Namba 414, Mamlaka hiyo iliundwa kwa lengo la kuhakikisha huduma za maji, umeme, gesi asilia na mafuta zinaimarika kwa kusimamia ubora, upatikanaji wake na kwa bei stahiki kwa manufaa ya wadau wote na taifa kwa ujumla.

“Kwa upande wa sekta ya maji, majukumu ya EWURA yameainishwa katika sheria ya EWURA na sheria ya Maji na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2019, ambayo ni kutoa leseni na kusimamia utekelezaji wa leseni, kwa mfano IGUWASA ina leseni ya EWURA hivyo ni wajibu wa Mamlaka ya maji Igunga kutekeleza matakwa ya leseni hiyo,” amesema Lweno.

” Maombi yaliyowasilishwa EWURA kutoka Mamlaka ya maji mjini Igunga ni maombi yaliyozingatia matakwa ya sheria ya kuzitaka Mamlaka za maji nchi nzima kufanya mapitio ya gharama zake baada ya miaka mitatu ili kutathmni bei ya maji na kuziwezesha mamlaka kutoa huduma bora za maji kwa wateja wake.”

Aidha Lweno amebainisha kuwa mkutano huo ni muhimu kwa wana Igunga, ambapo maoni yao yataisaidia EWURA kufikia uamuzi wa haki juu ya marekebisho ya bei ya maji.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya Sauda Mtondoo, ameipongeza EWURA kwa kutoa nafasi kwa wananchi kushiriki kutoa maoni juu ya ombi la Mamlaka ya maji mjini Igunga la kurekebisha bei, na kueleza kuwa, kwa kufanya hivyo itasaidia wananchi kuendelea kupata huduma bora.

” Ili kujua Mamlaka ya maji mjini Igunga imetoa huduma bora inatakiwa kutoa taarifa thabiti kwa wakati kwa watendaji wake yaani EWURA na kwa wananchi, kwa upande wa watumiaji wa huduma ya IGUWASA wana wajibu wa kuhakikisha wanalipia huduma kikamilifu na kwa wakati ili kuiwezesha Mamlaka kurudisha gharama za mtoaji huduma kwa lengo la kuwa na huduma endelevu, hivyo hizi ni jitihada za EWURA kuhakikisha inasimamia utekelezaji wa maadili yake moja wapo ikiwa ni uwazi,” amesema Mtondoo.

Ameendelea kusema kuwa, ” Niwaombe sana wananchi wote mliohudhuria mkutano huu kama wadau, sisi ni wawakilishi wa wale ambao hawajapata fursa ya kufika, kwa hiyo ni imani yangu kwamba mtakwenda kuwa chachu hata pale mabadiliko yatakapofanyika kwa kusema kwamba tulishiriki katika kutoa maoni, kwa hiyo maoni yenu yatakuwa na mchango mkubwa sana kwa EWURA watakapo kwenda kutathmini ili kupata gharama sahihi zitakazokuwa na mafanikio kwetu sisi watumiaji wa huduma na kwa watoa huduma.”

Meneja wa IGUWASA Mhandisi Hamphrey Mwiyobela akitoa maelezo kuhusu ombi la kurekebisha bei za kutoa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Igunga amesema kuwa wameomba marekebisho ya bei za maji kwa mwaka wa fedha 2023/2024, 2024/2025 na 2025/2026 kwa kuzingatia mpango kazi wao wa biashara, ambapo ameeleza sababu za kurekebisha bei za huduma ya maji ni ongezeko la gharama za uendeshaji, matengenezo ya miundombinu pamoja na gharama za uwekezaji.

” Katika miaka mitatu ijayo Mamlaka imepanga kutekeleza shughuli mbalimbali ambazo zitafanya kuboresha huduma ya maji safi na usafi wa mazingira hapa mjini Igunga ambazo ni kuongeza mtandao wa maji kwa kilometa 24, kuondoa bomba chakavu kilometa 19.2, kupunguza upotevu wa maji, kubadili dira 1000, kuongeza eneo la kutibu maji taka kutoka ekari 10 hadi kufikia ekari 50 na kutoa mafunzo kwa watumishi ya muda mfupi na mrefu,” akisema Mhandisi Mwiyobela.

Mwiyobela amezitaja bei ambazo wameomba zitumike kwa miaka mitatu ijayo kuwa ni kwa wateja wa majumbani kutoka bei ya sasa ya shilingi 1,666 ambapo bei mpya kwa mwaka 2023/2024 iwe ni 1,786, 2024/2025 ni 1,886 na 2025/2026 iwe 1,986, huku ada ya kurejeshewa huduma ikibakia ni shilingi 15,000 pia bei hizo zitabadilika kwa Taasisi, sehemu za biashara, Viwanda, Magati na kwa wateja wa jumla.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika mkutano huo na kutoa maoni yao Mbogo Athumani, Edward Magembe, Rosmery John, Epifania Labia, Charles Bundala BBC na Selemani Majilanga wameipongeza IGUWASA na EWURA kwa kuona umuhimu wa kuwashirikisha na kutoa maoni yao juu ya maombi ya bei hizo mpya na kuunga hoja kutokana na sababu ambazo zimetolewa na IGUWASA.

Kwa upande wao wawakilishi kutoka Baraza la ushauri la Serikali (GCC) Thabiti Dokodoko na Hawa Ng’humbi kutoka baraza la watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa na EWURA (CCC) wameiomba EWURA kuzingatia maoni yao na ya wananchi kutokana na ombi la mapendekezo yaliyotolewa kufuatia wasilisho la IGUWASA kuwa yatazingatiwa wakati wa majumuisho ya kupitia maombi hayo ya bei ili kuwepo na bei za huduma zenye uhalisia na zisizo muumiza mtumiaji.