January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

IGUWASA  yaanika mafanikio yake mwaka wa fedha 2022/2023

Na Lubango Mleka, Timesmajira Online 

KATIKA kifikia adhima ya Serikali ya kumtua mama ndoo kichwani, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Igunga (IGUWASA) imetafsiri sera hiyo kwa vitendo, ambapo imefanikiwa kutoa huduma ya maji kwa wakazi wa Igunga na maeneo ya jirani kwa asilimia 98 huku lengo lake kuu kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kutoa huduma hiyo kwa asilimia 100.

IGUWASA inatoaa huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Kata ya Igunga na Kata zingine za pembezoni zikiwemo Nguvumoja katika kijiji cha Mwalala, Mbutu, Mwamashimba na Isakamaliwa katika eneo la Hindishi.

Eneo hilo lina jumla ya watu 141,459 kwa sasa sawa na  wastani wa watu 6 kila kaya  kutokana na takwimu za Sensa ya mwaka 2022 ambapo IGUWASA imefikisha huduma ya maji kwa  watu takribani 123,625 sawa na asilimia 87.4 Kata ya Igunga.

Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Mjini Igunga, Mhandisi Hamphrey Mwiyobela akizungumzia mafanikio ya Mamlaka hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024.

IGUWASA inatoa ya huduma ya maji kwa asilimia 98 ya wakazi wote wa mji wa Igunga, inatoa huduma zake kupitia magati ya kuchotea maji, maunganisho ya nyumbani,taasisi, maeneo ya biashara na viwanda, ambapo ina jumla ya wateja 9,925 mpaka kufikia mwezi Juni, 2023 na mahitaji ya maji ni lita za ujazo 4,400 kwa siku.

Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Igunga, Mhandisi Hamphrey Mwiyobela anasema kuwa dira na dhamira yao ni kuwa miongoni mwa mamlaka zinazotoa huduma bora na endelevu ya majisafi na usafi wa mazingira nchini huku dhamira ikiwa kutoa huduma ya maji yakutosha na inayokidhi viwango vya ubora pamoja na huduma ya usafi wa mazingira.

UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAJI IGUNGA.

“Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira mjini Igunga mbali na kusimamia na kutoa huduma ya maji na usafi wa mazingira pia imetekeleza miradi miwili ya kuboresha huduma ya majisafi na salama katika vijiji vya Mwabakima, Jogohya, Mwamashimba na Mwalala,”anasema Mhandisi Mwiyobela.

Mwabakima, Jogohya, Mwamashimba na Mwalala ni miongoni mwa vijiji katika Wilaya ya Igunga ambavyo vilikuwa vinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa kipindi cha muda mrefu.

Hivyo Wizara ya Maji kupitia IGUWASA imetekeleza miradi ya upanuzi wa mtandao wa majisafi na salama ili kuwezesha kupata maji  yaliyokidhi viwango vya kwa ajili ya matumizi ya binadamu.

“Mamlaka yetu imefanikiwa kutekeleza  na kusimamia miradi ambayo ni mradi wa upanuzi wa mtandao wa majisafi na salama kutoka kijiji cha Mwanzugi mpaka kijiji cha Mwalala kilometa 8, uliogharimu kiasi cha milioni 328, mradi ambao unanufaisha wakazi wa kijiji cha Mwalala wapatao 5,730,” anasema Mwiyobela.

Pia anaeleza kuwa mradi wa upanuzi mtandao majisafi na salama  kutoka vijiji vya Mwabakima, Jogohya na Mwamashimba kilometa 17 umegharimu kiasi cha shilingi milioni 824,utanufaisha wakazi takribani 10,431 katika vijiji hivyo, aidha miradi yote inatekelezwa kwa utaratibu wa  force account chini ya usimamizi wa mamlaka  hiyo.

MAFANIKIO YA MAMLAKA 2022/2023.

Mamlaka hiyo imefanikiwa katika maeneo mbalimbali ya utoaji wa huduma katika Kata ya Igunga, Isakamaliwa, Mbutu na baadhi ya vijiji vya Kata ya Mwamashimba.

” Mamlaka imefanikiwa kuongeza maeneo ya utoaji wa huduma ya majisafi kwa kuongeza Kata ya Nguvumoja katika kijiji cha Mwalala, Kata ya Mwamashimba kwa vijiji vya Mwamashimba  na Jogohya, Kata ya Isakamaliwa pamoja na Kata ya Mbutu kijiji cha Mwabakima, hivyo kufanya IGUWASA kuwafikishia huduma bora na ya uhakika watu takribani 123,625 ambao ni sawa na asilimia 87.4, waliopo katika eneo lote hilo kupata huduma kupitia magati, maunganisho ya nyumbani, taasisi, maeneo ya biashara na viwanda,” amebainisha Mhandisi Mwiyobela.

Moja ya gari ambalo lilikuwa linatoa huduma kwa wananchi wa pembezoni mwa mji wa Igunga kabla ya kufikishiwa huduma ya majisafi na salama na IGUWASA jambo ambalo limewasaidia wananchi kutumia muda mchache kupata huduma hiyo ya maji.

Aidha anasema kuwa IGUWASA  imefanikiwa kupata tuzo ya kuwa mshindi wa pili kati ya mamlaka 57 za ngazi ya wilaya na miji midogo katika utoaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira, tuzo hizi zinatolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA).

Pia IGUWASA imefanikiwa kuongeza mtandao wa majisafi kutoka kilometa 317 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia kilometa 348 sawa na ongezeko la kilometa 31 hadi kufikia Juni, 2023, kuongeza wateja wapya kutoka 9085 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia wateja 9,925 kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Mamlaka imefanikiwa kudhibiti upotevu wa maji (Non Revenue Water) kutoka asilimia 26 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia asilimia 17.6 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 hivyo imevuka lengo la asilimia 24, kupungua kwa upotevu huo ni kutokana na kuongeza idadi ya watumishi wakiwemo mafundi, kubadilisha dira chakavu  za maji 314 kwa mwaka wa fedha 2022/2023, ubadilishaji wa miundombinu chakavu ya bomba na kupelekea upatikanaji wa maji kwa saa 24.

“Mamlaka imefanikiwa kununua na kufunga dira za maji za malipo ya kabla(Luku) kwa baadhi ya wateja wetu kwa hatua za awali za kupima ufanisi (piloting) na zimeonesha ufanisi mkubwa na mamlaka inatarajia kuingiza katika mipango yake ya ununuzi wa dira hizi zaidi,” anasema Mhandisi Mwiyobela.

MPANGO WA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA WA FEDHA 2023/2024.

Wizara ya Maji kupitia IGUWASA kwa mwaka wa fedha 2022/2023 imetenga kiasi cha  bilioni 1,kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kutibu maji taka (Faecal Sludge Treatment Facilities) na tayari mkandarasi yupo site katika kijiji cha Ipumbulya kwa hatua za kuanza kutekeleza mradi na utakuwa na uwezo wa kutibu majitaka lita za ujazo 1100 kwa siku.

“Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali kupitia Wizara ya maji imetenga kiasi cha  milioni 200 kwa ajili ya ukarabati (Rihabilitation of Water Production System) kwa lengo la kukarabati chanzo cha maji katika bwawa la Bulenya ili kuongeza uzalishaji kutoka lita za ujazo 1000 kwa siku hadi lita za ujazo 4000 kwa siku,” anabainisha Mwiyobela.

Mpango mwingine wa IGUWASA ni kuongeza mtandao wa majisafi (Water Distribution Network) ambapo Serikali imetoa kiasi cha  milion 800 katika bajeti ya mwaka wa fedha2023/2024 kwa ujenzi wa mtandao wa maji kilometa 12 kutoka kijiji cha Makomelo mpaka kijiji cha Mgongoro, pia kupitia mapato ya ndani imetenga fedha kwa ajili ya kuongeza mtandao wa maji kutoka vijiji vya Mwanzugi, Mwamaganga, Majengo, Mwabakima na Mwanyalali.

Hata hivyo Mamlaka pia imepanga kukabiliana na changamoto ya upotevu wa maji ambao kwa sasa ni asilimia 17.6 na ikiwa imevuka lengo la asilimia 24, ambapo wamedhibiti upotevu wa maji kwa kubadilisha kilometa 5, za mitandao ya bomba chakavu na kubadilisha dira za maji zinazo haribiwa na wateja, kuboresha maslahi ya watumishi na vifaa wanavyofanyia kazi ili kuongeza ufanisi na weledi wa kuzingatia mipango ya mamlaka.

“Mipango yetu tumefanikiwa kufunga dira kumi za malipo ya kabla (Luku) kwa baadhi ya taasisi kwa ajili ya majaribio kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa makusanyo ya mauzo ya maji, hivyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 tumejipanga kuongeza dira za malipo ya kabla 40,”.

Dudu Kitoma ni mwananchi wa wilaya ya Igunga ambaye anazungumzia hali ya maji ilivyokuwa kipindi cha nyuma na kwa sasa huku akiipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya usimamizi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na  Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Igunga.

“Huduma za maji zimeboreshwa sana, hivi ninavyo ongea na wewe, nimefanya mchakato wa kuvutiwa maji, jana nilijaza fomu na leo nimepatiwa namba ya malipo nimelipia kama saa moja lililopita na sasa tayari nina dira ya usomaji maji yenye jina langu, kwa kweli niwapongeze IGUWASA kwa kutujali wana Igunga,” amesema Kitoma.

Huku Rosemary Hengele akibainisha hali ilivyokuwa miaka ya nyuma na sasa, ” kupitia maji haya kutoka ziwa Victoria kwa kweli akina mama tumeimarika kiuchumi na hata ndoa zetu zimekuwa bora, maana tulitumia muda mwingi kufuata maji mtoni umbali wa kilometa saba au nane kutoka mjini na ilitubidi kuamka saa kumi alfajiri kuwahi foleni ya maji, lakini kwa sasa ninatumia dakika tu kupata maji kwani kila nyumba ina bomba la maji, namshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na IGUWASA kwa kutupatia maji haya kutoka mkoani Mwanza na leo tunayapa Igunga bila ya shida,”.