December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Biharamulo, Adia Rashid Mamu (kulia) akimkabidhi, Idrissa Songoro fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea ubunge katika Jimbo la Biharamulo mkoani Kagera.

Idrisa Songoro asema yupo tayari kwenda kushirikiana na Wanabiharamulo kuharakisha maendeleo

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Biharamulo

MJASIRIAMALI na mkulima, Idrisa Twaibu Songoro amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania nafasi ya ubunge katika Jimbo la Biharamulo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Songoro ni miongoni mwa wakulima ambao majina yao si geni miongoni mwa wakazi na wakulima wa maeneo mbalimbali nchini hususani wilayani Biharamulo mkoani Kagera kutokana na mbinu shirikishi ambazo huwa anazitumia kuwawezesha wakulima kufikia lengo la kuzalisha zaidi kwa ajili ya chakula na biashara.

Amesema kuwa, kutokana na demokrasia iliyopo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) anajiona anatosha kuwatumikia wana Biharamulo.

Amesema, akipata ridhaa ya chama na wananchi atashirikiana bega kwa bega na wananchi kuleta maendeleo na kuibadilisha Biharamulo.

“Nimeamua kutia nia, kuchukua fomu katika chama changu Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Biharamulo kwa nia na madhumuni ya kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na haki za msingi za mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi, kama ilivyoelekezwa na chama chetu.

“Lengo na madhumuni ya kuchukua fomu hii, ni kuweza kuleta changamoto, kulea mabadiliko kama Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi anavyosema kwamba, tuna Tanzania mpya, tuna CCM mpya, lakini kwa sisi watu wa Biharamulo tunasema tunahitaji Biharamulo mpya, na Biharamulo mpya tunaiona kutokana na jitihada za Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dkt.John Pombe Magufuli kwamba ameshatutengenezea miundombinu, ameshatengeneza sera bora za maendeleo kwa ajili ya sisi kuyafikia malengo, hivyo ninaamini nikipewa nafasi ninatosha kushirikiana na Wana Biharamulo kuyafikia maendeleo kwa kasi,”amesema Songoro.