November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Huyu sasa ndio Jaji Augustino Ramadhan, kama ulikuwa humfahamu

Na Mwandishi Wetu

Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani

JANA Aprili 28, mwaka huu Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani, alifariki Dunia katika Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu. Kifo cha Jaji Ramadhan kimeacha pigo kubwa kwa tasinia ya sheria, lakini pia kwa waumini wa Kanisa la Anglikana ambapo alikuwa Mchungaji.

Pamoja na mchango wake mkubwa kwa Taifa na nje ya mipaka ya nchi yetu, Watanzania wengi inawezekana hawajui historia yake. Historia ya Jaji Ramadhan ina mambo mengi ya kujifunza kwa wanadamu.

Jaji Augustino alizaliwa Desemba 28, 1945 akiwa mtoto wa pili katika familia ya watoto wanne. Familia yake ina majina mchanganyiko ya dini ya kiislam na kikristo, lakini familia hii ni ya kikristo madhehebu ya Anglikana.

Baba yake alikuwa Mwalimu Mathew Douglas Ramasdhan na mama yake, mkewe, Mwalimu Bridget Anna Masoud wakazi wa Kisima-Majongoo, Zanzibar.

Mwaka 1952 baba yake Mwalimu Mathew Ramadhani alihamishiwa Mpwapwa, Dodoma kwenda kufundisha, akiwa na familia yake, huku Jaji Augustono akiwa na miaka saba. Alihitimu elimu yake Wilayani Mpwapwa na kufaulu vizuri masomo yake ya shule ya msingi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Jaji Mkuu wa Tanzania Mstaafu Mhe. Augustino Ramadhani kabla ya kikao Ikulu jijini Dar es Salaam.Julai 3,2018. Picha ya Maktaba

Alichaguliwa kujiunga na shule maarufu iliyokuwa ikitayarisha vijana wa Tanganyika kuja kushika uongozi wa nchi Tabora Boys  kuanzia mwaka 1960 hadi kumaliza kidato cha sita mwaka 1965.

Akiwa shuleni hapo alijifunza mambo mengi ikiwemo kupiga piano ambapo pia alirithi kipaji cha babu yake ambaye pia alirithi jina lake, Augustino Ramadhani. Aidha, alijifunza “basketball” aliyoimudu sana kutokana na wajihi wake kwani “amekwenda hewani”.

Baba yake kufariki katika ajali ya treni  akiwa masomoni nchini Uingereza katika ajali ya treni katika kituo cha Guidebridge Ashton Under-Lyne: Inadaiwa kifo chake kilichagizwa na ubaguzi wa rangi ambao ulikuwa umetamalaki vilivyo nchini Uingereza wakati huo ambapo
inadaiwa alisukumwa na kukanyagwa na treni na akazikwa Southern Graveyard.

Licha ya uchungu mkubwa wa kufiwa na mzazi wake huyo aliyekuwa wa kupigiwa mfano kwa maadili, akili na utanashati, aliingiwa na hofu kubwa kuwa huo ndio ungekuwa mwisho wake kusoma kwa kukosa mtu wa kumlipia ada.

Jaji MKuu Mstaafu Augustino Ramadhani, akipiga kinada kanisani

Hata hivyo, aliweza kusoma na si tu kumaliza kidato cha sita bali pia kufaulu kwa kiwango cha juu.

Jaji Augustino alijiunga na Chuo Kikuu kusomea fani ya sheria, akiwa ni mmoja wa Watanzania wa mwanzomwanzo kusomea fani hii ya kipekee.

Kufyekelewa mbali na Rais Nyerere

Mwaka 1966 kulitokea mgomo wa kwanza mkubwa katika historia ya chuo hicho. Wanafunzi walikuwa wakipinga masharti ya kujiunga kwa lazma na JKT.

Ingawa kuna baadhi ya wanafunzi hawakushiriki mgomo huo akiwemo Jaji Augustino, Rais NYERERE (Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere) aligadhabishwa mno na kitendo hicho kisicho cha kizalendo, hivyo kuwafukuzilia mbali wanafunzi wote.

Wanafunzi hao, hata hivyo, walirejeshwa chuoni hapo mwezi Julai, 1967.

Kukata kadi ya TANU

Jaji Augustino alikata kadi ya TANU na akawa mwanachama wa  TANU Youth League, akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu, mwaka 1969 katika Tawi la Temeke.

Kumaliza Chuo Kikuu

Jaji Augustino alimaliza elimu ya Chuo Kikuu mwaka 1970 na kufaulu vizuri.

Kujiunga na JWTZ

Mwezi Machi 1970, baada ya kumaliza Chuo Kikuu, Jaji Augustino alijiunga na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Kuoa

Licha ya kuwa mkristo, Jaji Augustino alimuoa, Saada Mbarouk  MBAROUK, ambaye ni mwislam.Alioa Novemba 11, mwaka 1975.

Kuteuliwa Naibu Mwanasheria Mkuu ZNZ:

Mwaka 1978 ulikuwa ni mwaka wa mafanikio makubwa kwake. Mwanzoni mwaka 1978, Rais wa pili wa Zanzibar, Alhaj Abdou Jumbe Mwinyi, alimteua kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, kikiwa ni moja ya vyeo vya juu kisiwani humo.

Mwaka huo huo wa 1978, alipata shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kurudishwa JWTZ

Machi 1979, Augustino alirudishwa JWTZ na katika vita ya Kagera iliyorindima mwaka huo alipelekwa vitani ambako jukumu lake kubwa lilikuwa kuendesha mahakama za kijeshi.

Kuteuliwa Jaji Mkuu ZNZ

Mwezi Januari 1980,  Jaji Augustino liapishwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, akiwa Luteni Kanali. Alihudumu cheo hicho hadi mwaka 1989.

Kuteuliwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania

Juni 23, 1989, Rais wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa TZ, Alhaj Ali Hassan Mwinyi alimteua Jaji Augustino kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania.

Kujiondoa Uanachama wa CCM

Jaji Augustino alijiondoa uanachama wa CCM mwaka 1992 baada ya mabadiliko ya Katiba ya nchi yaliyokataza majaji na wanajeshi kuwa wanachama wa vyama vya siasa.

Kuteuliwa M/Mwenyekiti NEC

Mwaka 1993, Rais Mwinyi alimteua kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Alihudumu kwenye cheo hicho hadi mwaka 2003.

Kustaafu Uanajeshi

Mwaka 1997, alistaafu rasmi JWTZ akiwa na cheo cha Brigedia Jenerali na kuagwa kwa heshma zote za kijeshi.

Kuteuliwa Jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki

Jaji Augustino aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki Novemba, 2001 na kuhudumu hadi mwaka 2007.

Kuteuliwa M/Mwenyekiti ZEC

Jaji Augustino aliteuliwa Makamu wa Mwenyekiti Tume ya Uchaguzi, Zanzibar (ZEC) mwaka 2002 hadi 2007.

Kusomea Uchungaji

Jaji Augustino alisomea uchungaji Chuo Kikuu cha London nchini Uingereza ambapo mwaka 2004 alipata shahada ya uchungaji ( a Bachelor of Divinity).

Kuteuliwa Jaji Mkuu wa Tanzania

Jaji Augustino alipata heshma ya kipekee alipoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania mwaka 2007 na akahudumu kwenye cheo hicho hadi Desemba  27, 2010 baada ya kufikisha miaka 65, ambao ni muda wa kustaafa kwa lazima kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

Kuteuliwa Jaji wa Mahakama ya Afrika

Mwaka 2010, aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu.

Kurejea CCM

Jaji Augustino baada ya kustaafu, alirejea uanachama wa CCM mwezi Septemba 2011 katika Tawi la CCM, Oysterbay.

Kutunukiwa Tuzo Maalum na Balozi wa Marekani

Februali 23, 2012, alitunukiwa Tuzo Maalum “Dr. Martin Luther King Award” na Balozi wa Marekani,  ALFONSO LENHARDT kutonaka na utumishi wake uliotukuka na hivyo kuwa Mbongo wa 13 kupokea Tuzo hiyo mujarab.

Kuteuliwa M/Mwenyekiti Tume ya Katiba

Aprili 7, 2012, Rais Kikwate alimteua Jaji Augustino kuwa Makamu Mwenyekiti Tume ya Katiba ambapo alitoa mchango mkubwa.

Kusimikwa Mchungaji

Desemba 28, 2013,  Jaji Augustino alitawazwa kuwa Mchungaji wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar baada ya kuwa Shemasi kwa miezi sita. Mchungaji Augustino alitawazwa katika kanisa la Anglikana lililopo minara miwili, Unguja.

Kuteuliwa RAIS wa Mahakama ya Afrika:

Septemba 14, 2014, alichaguliwa Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu baada ya kuonesha uwezo mkubwa akiwa jaji wa kawaida wa mahakama hiyo ambapo katika uchaguzi alipata kura 9 na hivyo kumzidi mpinzani wake aliyeambulia kura  nne .

Alihudumu katika cheo hicho hadi alipomaliza ngwe yake Jumapili ya Septemba 3, 2016.

Rais JK Amtunuku Nishani

Desemba 9, 2014, katika maadhimisho ya miaka 53 ya uhuru wa Tanganyika, Rais wa awamu ya nne, Kikwete alimtunuku Nishani Maalumu ya utumishi uliotukuka.

Kuwania urais

Jaji Augustino aliushangaza umma Juni 15, 2015 pale jijini Dodoma alipochukua fomu ya kugombea urais kupitia CCM na kuwa mmoja wa wagombea 42.

Rekodi za Kipekee

Moja, ni Mtanzania pekee kushika wadhifa wa Jaji Mkuu Zanzibar na Tanzania, ni Mtanzania wa kwanza kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Mtanzania pekee kuwahi kuwa Rais wa Mahamaka ya Afrika ya Haki za Binadamu.

Pia ni Mtanzania pekee kuwa Jaji Mkuu kisha Mchungaji, ni Mtanzania pekee kuwa Jaji Mkuu na Brigedia Jenerali, ni Mtanzania pekee aliyejaliwa talanta nyingi kwenye tasnia tofauti (Jurist, Basketballer, Pianist, Army officer & Pastor). Mchungaji Augustino
aliwahi kuwa Mwenyekiti wa ” Tanzania Basketball Association”.