Na David John, TimesMajira Online
ZAIDI ya watu 2,000 wakazi wa kijiji cha Nyamishiga Kata ya Lunguya Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama Mkoani shinyanga, wameondokana na adha ya kutembea umbali wa kilomita 15 kufuata huduma za Afya Lunguya baada ya Mgodi kujenga Zahanati kijijini kwao.
Ujenzi wa kituo cha afya ni juhudi za kikundi cha Wanawake wanaojishughulisha na shughuli za Uchimbaji wa Dhahabu katika Halmashauri ya Msalala ambacho kilipewa dhamana na serikali ya kusimamia maduhuri na tozo mbalimbali kwenye eneo lenye mfumuko wa Madini ya Dhahabu (RUSH) katika kijiji hicho.
Akizungumzia ujenzi wa zahanati hiyo hivi karibuni wilayani humo ambayo imekamilika kwa asilimia 80 Semeni John mwenyekiti wa Mgodi huo amesema kuwa wanajivunia kujenga Zahanati ya Kijiji chao cha Nyamishiga.
“kupitia CSR ya shilingi Milion 200 wamekusanya na kwamba Zahanati hiyo bado haijakamilika ipo kwenye asilimia 80″amesema Semeni.
Naye katibu wa Mgodi huo, Hilda Jackson amesema kuwa tangu wapewe usimamizi wa RUSH wameweza kukamilisha Ujenzi wa Zahanati hiyo kwa asilimia 80, na kuahidi kuendelea kuhamasisha wanawake kujiingiza kwenye shughuli za Uchimbaji wa Madini ya Dhahabu.
Akizungumza kwenye eneo la Zahanati hiyo hivi karibuni kwa niaba ya Wananchi wa Kijiji cha Nyamishiga Diwani wa Kata ya Lunguya Benedicto Manwari amesema kuwa wananchi wamefurahishwa na mgodi huo kuangalia eneo muhimu la huduma ya wananchi wote.
“Changamoto ya wananchi ni kutembea umbali mrefu Kwenda katani kutafuta matibabu inakwenda kumalizika, ambapo mpaka sasa wananchi wanapata huduma kwa taabu sana wanalazimika kutembea urefu wa kilomita 15 kwenda Lunguya Katani jambo ambalo nyakati za usiku ni shida wajawazito wanaofikia muda wa kujifungua ikitokea amekamatwa na uchungu usiku ni shida sana,” amesema Diwani enedicto Manwari
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Msalala Flora Sagasaga akizungumzia ujenzi huo amesema kuwa uwepo wa zahanati hiyo utasaidia wananchi wa Nyamishiga kupunguza mwendo wa kufuata huduma mbali wakiwamo na wachimbaji wadogo wanaofanya shughuli zao kwenye mgodi huo pindi wanapopata majeraha madogomadogo.
Hamza Tandiko ni mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wadogo Mkoa wa Shinyanga amesema kuwa wakina mama wachimbaji katika mgodi huo wameweza kuchangia CSR kiasi cha shilingi Milioni 203, na kuiomba serikali kupitia tume ya Madini iwarasimishe hawa wakinamama iwapatie leseni ya Uchimbaji ili wakusanye vyema maduhuli ya serikali pamoja na kuendelea kunufaisha wakazi wa Kijiji na maeneo mengine.
Kwa upande wake Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Kimadini Kahama Mhandisi Jeremia Hango akijibu ombi la leseni amesema kuwa yeye siyo msemaji wa mwisho kuhusu suala la leseni isipokuwa ombi lao atalifikisha kwa mhusika wa kitengo cha leseni makao makuu Jijijini Dodoma huku akikiri kuwa wanawake hao iwapo watapata leseni watachimba kwa bidi na tija zaidi.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini