November 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

HTM wachimba visima saba kukabiliana na uhaba wa maji Handeni

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Korogwe

KATIKA kukabiliana na shida ya maji inayowakabili wananchi wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM), imechimba visima virefu saba ili kukabiliana na uhaba wa maji.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Oktoba 18, 2022, Mkurugenzi Mtendaji wa HTM, Mhandisi Yohana Mgaza alisema wameamua kujenga visima hivyo katika maeneo tofauti, na maji yatakayopatikana yataingizwa kwenye mfumo wa mabomba ya Mradi wa HTM.

“Visima saba tulivyojenga, tunataka vitumike kuzalisha maji ambayo tutayaweka kwenye matenki yaliyopo ndani ya Mradi wa Handeni Trunk Main (HTM). Nia yetu ni kuona maji hayo yanapunguza uhaba wa maji kwa wananchi, na kuweza kuzalisha huduma ya maji kwa asilimia 70 kwa wananchi wa Handeni.

“Visima hivyo tumejenga kwenye vijiji tofauti ambapo matenki ya Mradi wa HTM yapo karibu. Na visima hivyo vipo Kijiji cha Malezi, Kata ya Malezi. Kijiji cha Mankinda, Kata ya Mabanda, Bwawani katika Kata ya Chanika. Ndelema, Kata ya Kwediamba, Kijiji cha Kwachaga,Kata ya Kwachaga. Kijiji cha Komkonga eneo la Hoza katika Kata ya Komkonga, na kisima cha saba kinajengwa Kijiji cha Kabuku Nje, Kata ya Kabuku Nje” alisema Mhandisi Mgaza.

Mgaza alisema, wakati wanashughulikia changamoto hiyo kwa mipango ya muda mfupi, tayari mradi huo wa HTM upo kwenye mpango wa Mradi mkubwa wa maji wa miji 28 nchini. Na tayari usanifu umeanza kwenye Mradi wa Maji HTM, na utakamilika Desemba, mwaka huu, na ujenzi kuanza Januari, mwakani.

Alisema, mradi huo wa miji 28, utaondoa tatizo la maji kwenye wilaya yote ya Handeni, lakini pia ukinufaisha miji ya Korogwe, Muheza na Pangani, huku chanzo cha maji cha mradi huo ukiwa ni Mto Pangani.

“Pamoja na malengo ya muda mfupi kukabiliana na tatizo la maji, pia Serikali inaleta mradi mkubwa wa miji 28. Mradi huo utakuwa wa sh. bilioni 200, na utahudumia mtandao mzima wa maji wa Mradi wa HTM, lakini utakwenda kwenye miji ya Korogwe, Muheza na Pangani.

“Kwa sasa Mradi wa HTM unazalisha lita milioni nne (4) kwa siku, lakini kutokana na ukarabati utakaofanyika, utaweza kuzalisha lita milioni 52 kwa siku, hivyo kuondoa shida ya maji kabisa Wilaya ya Handeni, miji ya Korogwe, Muheza na Pangani” alisema Mgaza.

Tenki la maji lenye mnara wa mita sita, na ujazo wa lita za maji 100,000, limejengwa kwenye Mradi wa Maji Majani Mapana, Kijiji cha Kabuku Ndani. Mradi huo uliogharimu sh. milioni 260, unajumuisha kisima, tenki, mabomba yenye urefu wa mita 6,600 na vilula 11.
Ujenzi wa tenki la Mradi wa Maji Kwamagome, Kata ya Kwamagome, Halmashauri ya Mji Handeni. Tenki lina ujazo wai lita 100,000. Mradi huo umekamilka na wananchi wanapata huduma ya maji, huku ukigharimu sh. milioni 244, na umejumuisha kisima kirefu, tenki, mabomba urefu wa mita 8,200 na vilula tisa. Maeneo yanayonufaika ni eneo la Mtaa wa Kwamagome na Hedi.
Moja ya kituo cha kuchotea maji (Kilula) Kwamagome.
Mradi wa Maji Mabanda, Kata ya Mabanda, ukijumuisha tenki lenye ujazo wa lita 100,000 kwenye mnara wa mita 12, urefu wa bomba ni mita 15,000, vilula 16, na gharama ya mradi ni sh. milioni 671. Mradi umekamilika na wananchi wanapata huduma ya maji.
Mkurugenzi Mtendaji wa HTM, Mhandisi Yohana Mgaza, akizungumza na mwandishi wa habari leo Oktoba 18, 2022 ofisini kwake. (Picha na Yusuph Mussa).