January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

HTM kumaliza tatizo la maji Handeni na Korogwe

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM) ipo kwenye mpango wa muda mfupi, kati na mrefu ili kumaliza tatizo la maji kwa Wilaya ya Handeni, Mji wa Korogwe na Mji wa Mombo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HTM Mhandisi Yohana Mgaza,kwenye mafunzo ya siku mbili kati ya viongozi wa CCM ngazi ya wilaya za Mkoa wa Tanga na Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Tanga, yaliyofanyika mjini Korogwe.

Mhandisi Mgaza amesema hatua za muda mfupi ili kuendelea kutoa huduma kwa wananchi, HTM inaendelea kutumia vyanzo vyote vilivyopo ili kusaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa maji pamoja na kuongeza muda kwa siku ya upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo ya huduma, kufanya manunuzi ya pampu za akiba katika vituo vya kusukuma maji.

Lakini pia, HTM imeomba fedha Wizara ya Maji kwa ajili ya kujenga miradi ya maji katika maeneo ya Komkonga, Kwachaga, Chogo, Mkwajuni na Kwediyamba ili kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi, kubadili Dira za maji (Mita) ambazo ufanisi wake umepungua na kuboresha miundombinu ya kusambaza maji kwa kulaza bomba lenye urefu wa kilomita 24.9 katika Mji wa Korogwe..

“Hatua za muda wa kati ni kutekeleza ujenzi wa Mradi wa Maji Segera- Kabuku kwa kujenga chanzo kipya katika eneo la Mkumburu, kujenga mtambo wa kutibu na kuchuja maji, kulaza bomba kuu, kulaza bomba la kusambazia maji, kujenga tenki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 2,000,000, kufanya ujenzi wa miradi kwa kutumia visima virefu katika maeneo ya Kwachaga, Chogo, Komkonga, Mkwajuni, Kwediyamba, ili kuongeza upatikanaji wa huduma ya Maji.

“Kushirikiana na Ofisi ya RUWASA Wilaya ya Handeni kukamilisha kujenga bwawa
la kuhifadhi maji la Kwenkambala, kufunga pampu mpya na kulaza mtandao mpya wa mabomba ya kutoa maji katika Mji wa Handeni, kufanya ujenzi wa miradi kwa kutumia visima virefu katika maeneo ya Kwediyamba na Mkwajuni ili kuongeza upatikanaji wa huduma ya Maji katika Mji wa Handeni”amesema Mhandisi Mgaza.

Mhandisi Mgaza amezitaja hatua za muda mrefu kuwa ni kufanya ukarabati na upanuzi wa mradi kwa kuongeza uzalishaji pamoja na miundombinu kupitia Mradi wa Maji Miji 28, ambapo hadi sasa mkandarasi yuko eneo la mradi anaendelea na ujenzi wa Dakio (Intake), Chujio (Water treatment Plant), ujenzi wa matenki na ulazaji wa mabomba, ambapo mpaka sasa amelaza jumla ya kilomita 90 kati ya 188.

Ujenzi wa Mradi wa Maji Segera- Kabuku, ambapo hadi sasa mkandarasi yuko eneo la mradi anaendelea na ujenzi wa Dakio (Intake), Chujio (Water treatment Plant), ujenzi wa tenki la lita 2,000,000 na ulazaji wa mabomba, ambapo mpaka sasa amelaza jumla ya kilomita 9.51 kati ya kilomita 26. Ujenzi wa mradi wa maji kwa kutumia chanzo cha Mto Ndemaha ambapo litajengwa dakio na kulaza bomba lenye urefu wa kilomita 21hadi mjini Korogwe, ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lenye uwezo wa kujaza lita 2,000,000 eneo la Kwamkole, Korogwe.

Ujenzi wa miundombinu ya kusafisha, kuchuja na kutibu maji (Water Treatment
Plant) eneo la Kwamkole, Korogwe ili kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama. Ujenzi wa Maabara ya maji Kwamkole, Korogwe, ambapo hadi sasa mkandarasi anaendelea na kazi ya ujenzi, ujenzi wa Chujio (Water Treatment Plant) pamoja na Ofisi ya Mamlaka ya Maji na kununua vitendea kazi katika Kanda ya Mombo.