Na Faraja Mpina, TimesMajira Online, Dodoma
NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iliyokuwa Sekta ya Mawasiliano,Dkt.Jim Yonazi ametembelea na kukagua hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika hospitali ya Uhuru inayojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, jijini Dodoma.
Dkt.Yonazi amekagua Ujenzi wa wa mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, vyumba maalumu ambavyo mifumo ya TEHAMA itafungwa na kuunganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano pamoja na upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya sauti na data ikiwemo mitandao ya simu za mkononi
Dkt.Yonazi amesema kuwa lengo la kufanya ukaguzi huo ni kuhakikisha kuwa huduma bora za mawasiliano katika hospitali hiyo zinapatikana na zinazingatia matumizi ya kisasa ya TEHAMA
“Jukumu letu la msingi ni kuwezesha sekta mbalimbali kutumia TEHAMA ikiwemo Sekta ya Afya, lengo ni kuhakikisha Sekta ya Afya inatumia TEHAMA katika kutoa huduma zake kwa wananchi ikiwemo elimu ya afya kwa njia ya mtandao”, amesisitiza Dkt.Yonazi
Naye Meneja wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Mkoa wa Dodoma, Simon Marwa amesema kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo umefikia kiwango cha asilimia 60 na utakamilika na kuwa tayari kutumika mara hospitali hiyo itakapoanza kutoa huduma.
Katika hatua nyingine Marwa amesema kuwa TTCL inajipanga kutekeleza agizo la Dkt. Yonazi la kuhakikisha huduma za intaneti zinapatikana kwa wananchi watakaofika katika hospitali hiyo pamoja huduma za kuweka na kutoa pesa mtandaoni kwa kutumia T-Pesa
Aidha, Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto wa Wilaya ya Chamwino, Neema Mlula amesema kuwa kuwekwa kwa miundombinu hiyo na mifumo ya TEHAMA katika hospitali hiyo kutawezesha utoaji wa huduma za afya, kukusanya takwimu na kuhifadhi kumbukumbu za wagonjwa
Ameongeza kuwa, mifumo ya TEHAMA itaunganishwa kwenye vitengo nane vya hospitali hiyo ili kufanikisha utoaji wa huduma bora na kwa wakati, huku akivitaja vitengo hivyo kuwa ni wagonjwa wa nje, idara ya mionzi, maabara, kitengo cha dawa,idara ya macho, idara ya afya ya kinywa na meno, idara ya utawala na idara ya afya ya uzazi na mtoto.
More Stories
Samia, Mwinyi wawapa miezi mitatu wawekezaji
Tanzania,Uingereza kushirikiana katika kuendeleza madini Mkakati
Kamati ya Mfuko wa Jimbo Musoma Vijijini yagawa vifaa vya ujenzi