March 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kuanzisha matibabu ya upasuaji moyo

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda Mbeya imejiandaa kuanzisha huduma ya matibabu ya kibingwa bobezi ya pasuaji wa moyo, mishipa ya damu na kifua,ikiwa ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za afya katika Nyanda za Juu Kusini na lango kuu la Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, SADC.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo,Petro Seme, amesema hayo Machi 14,2025 Ofisini kwake wakati wa makabidhiano ya mkataba wa ununuzi wa mtambo wa kisasa wa Cathlab (Catheterization Laboratory) wenye uwezo wa kufanya uchunguzi na matibabu ya hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo, kwa mwakilishi wa mzabuni kampuni ya Computech ICS Tanzania Limited, Mhandisi Gilbert Sangu.

Tunatambua umuhimu wa mradi huu na jukumu lako katika kuhakikisha huduma hii ya kibobezi inapatikana kwa haraka, kuanzishwa kwa huduma hii kutasaidia kuokoa maisha ya watoto na watu wazima katika kanda hii. Ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa tunatekeleza kwa ufanisi ili wananchi waweze kupata huduma bora za matibabu.” amesema Petro Seme

Seme amesisitiza kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt.Samia Suluhu Hassan imewekeza kwa kiasi kikubwa katika miundo mbinu ya kisasa, Wataalamu wabobezi na vifaa tiba katika kuanzishwa kwa huduma hii muhimu na hivyo, hivyo mzabuni hana sababu ya kuchelewesha huduma hiyo kuanza. Aidha, ameweka wazi kuwa ni muhimu kwa mzabuni huyo kutoa taarifa mara kwa mara kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa ununuzi wa mashine hiyo ya Cathlab (Catheterization Laboratory).

Mhandisi Gilbert Sangu kutoka Computech amesema kuwa wanatambua kwamba uwekezaji huu wa Serikali ni muhimu na wa kipekee, hivyo kuahidi kutekeleza Majukumu hayo kwa ufanisi na kwa wakati ili kuhakikisha mashine ya Cathlab (Catheterization Laboratory) inafika Mbeya na kazi zake zinaanza haraka.

“Napenda kushukuru kwa fursa hii ya kipekee ya kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya.Ni heshima kubwa kwetu kuwa sehemu ya mradi huu wa maana ambao utabadilisha maisha ya watu wengi katika jamii yetu. tutahakikisha kuwa tunatoa taarifa za mara kwa mara kuhusu maendeleo ya mradi huu, kwani tunajua umuhimu wa uwazi na mawasiliano bora kwa pande zote,”Mhandisi Sangu.

Kwa sasa, ujenzi wa jengo jipya la kuwekea mtambo hiyo umekamilika kwa asilimia 70, ikiwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha huduma hizi zinaanza kwa haraka ambazo pia zitachochea maendeleo ya tiba utalii nchii.