Fresha Kinasa, TimesMajira Online, Musoma.
WANANCHI wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Mkoani Mara wameishukuru serikali kwa kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya hiyo, ambapo kwa Sasa imeanza kutoa huduma mbalimbali za afya.
Hospital hiyo imejengwa Katika Kitongoji Cha Kwikero Kijiji cha Suguti Katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ambapo uwekezaji uliotumiwa na Serikali upande wa ujenzi ni Shilingi Bil.3.53,huku uwekezaji wa vifaa tiba ukiwa ni zaidi ya Bil. 2,ikiwa na vifaa tiba vya kisasa . Mashine ya X-ray, Ultra Sound, Oxigen Plant na vifaa mbalimbali.
Wananchi hao wameyasema hayo Oktoba mosi, 2024, mbele ya Waziri Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene aliyefika kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Hospitali hiyo ambayo imeishaanza kutoa huduma kwa Wananchi.
Sadick Mohamed ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Suguti amesema kuwa, kuanza kutolewa kwa huduma za Afya katika hospitali hiyo ni faraja kubwa na mwarobaini kwa Wananchi ambao awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kwenda Mjini Musoma kupata matibabu yaliyohitaji uchunguzi mkubwa.
Rhoda Mafuru ambaye ni Mkazi wa Kitongoji cha Kwikonero amesema, kina Mama wajawazito hawatapata tabu, kwani huduma ya Ultrasound ambayo ni muhimu kwao. Kwa sasa wanaipata katika Hospitali hiyo na pia uhakika kwa kina mama Wajawazito kujifungua salama umeongezeka mara dufu.
“Tunashukuru juhudi za Mbunge wetu Prof. Muhongo kupambania hospital hii ambayo imekamilika kwa Sasa, tulikuwa tunalazimika kwenda Musoma Mjini wakati mwingine mtu hana pesa ya nauli na anahitaji huduma ya X-ray kwa hiyo mbali na pesa ya matibabu lazima awe na nauli lakini sasa hivi huduma hii tunaipata hapa kwa ubora.” amesema Zainabu Majura.
Naye Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof.Sospter Muhongo amesema, anaishukuru Serikali kwa kufanya Uwekezaji mkubwa wa kujenga Hospitali hiyo na kuweka vifaa tiba vya kisasa ambapo kwa sasa ni mkombozi kwa Wananchi wa Musoma Vijijini ambao walitamani kuwa na hospital ya hadhi hiyo kwa muda mrefu.
Amesema, Jimbo la Musoma Vijijini limeendelea kunufaika na fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo zinazotolewa na Serikali katika upande wa miradi ya elimu, afya na miundombinu jimboni humo.
Kwa upande wake Waziri Nchi Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene akiweka Jiwe la Msingi wa ujenzi wa Hospitali hiyo amepongeza waliofanya usimamizi wa mradi huo kwa ubora unaotakiwa.
Waziri Simbachawene amesema, serikali itaendelea kuhakikisha inatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inagusa maisha ya Watanzania sehemu mbalimbali hapa nchini.
More Stories
TAKUKURU,rafiki yanufaisha wananchi Mwanza
Mhandisi Samamba awasisitiza maafisa madini kusimamia usalama wa migoni msimu wa mvua
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa