Na Jackline Martin, TimesMajira Online
Wanawake wanaosumbuliwa na Fistula wametakiwa kutojificha kwa kuogopa aibu hivyo wajitokeze na wafike katika hospitali ya CCBRT kwaajili ya kupata matibabu
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 20,2022 jijini Dar es Salaam na Mganga mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Dkt.Rashid Mfaume wakati wa Maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kutokomeza fistula.
Akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema amezitaka Halmashauri zote za mkoa wa Dar es Salaam kuweka mikakati ya kuwatumia wahudumu wa Afya ngazi ya jamii kuwaibua wasichana na akina mama wenye matatizo ya fistula ili waweze kupatiwa matibabu.
Aidha Dkt. Mfaume amesema kaulimbiu ya mwaka huu inahamasisha zaidi fistula itokomezwe kwa kutibu wagonjwa wote waliopo na kuzuia wagonjwa wapya;
“Kaulimbiu ya mwaka huu inasema ‘Tokomeza fistula, wekeza katika kuboresha huduma za Afya na wezesha jamii’, kaulimbiu hii inataka fistula itokomezwe kwa kutibu wagonjwa wote waliopo na kuzuia wagonjwa wapya kwa kuboresha huduma za Afya na kuwezesha jamii”
Pia Dkt. Mfaume amesema matibabu ya fistula yanapatikana bila malipo kutoka kwa mgonjwa ikiwa ni pamoja na nauli ya kuja hospitali na kurudi nyumbani, na matibabu hayo yanapatikana mkoani Dar es salaam hapo CCBRT na Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Mbali na hayo Dkt. Mfaume amewataka Wananchi kuimarisha uhamasishaji ili wakina mama wote wanaoteseka na fistula mkoani Dar es salaam na Tanzania mateso yao yafikie ukomo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji mkuu wa CCBRT Brenda Msangi amesema tangu kuanza kwa mapambano ya fistula mwaka 2003 wamepiga hatua kubwa Kitaifa katika kutoa matibabu ya Fistula kwa maelfu ya akina mama wenye tatizo hilo ambapo zaidi ya akina mama 17,500 wamepatiwa matibabu CCBRT na katika hospitali washirika.
Aidha Brenda ametoa wito kwa Watanzania kutoa mchango katika kutokomeza fistula;
“Mwaka Jana tumetoka matibabu kwa akina mama 462 hii ni namba ndogo Sana ikilinganishwa na ukubwa wa tatizo, natoa wito kwa Watanzania wenzangu Kila mmoja wetu atoe mchango katika kutokomeza fistula, kama huna pesa mueleze mwanamke juu ya upatikanaji wa matibabu ya ugonjwa huu, kuwepo na sera zinazolenga kuboresha mazingira ya upatikanaji wa huduma bora za Afya ya mama na mtoto lakini pia sekta binafsi iwezeshe upatikanaji wa huduma hizi hapa nchini badala ya kuendelea kuwa tegemezi kwa wahisani kutoka nje”
Nao baadhi ya wagonjwa wa fistula wanaotibiwa katika hospitali CCBRT wametumia nafasi hiyo kuwataka akina mama walioathirika na ugonjwa huo kutojitomeza na kupatiwa matibabu kwani ugonjwa wa Fistula unatibika.
Tarehe 23 Mei ya Kila mwaka Tanzania huungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku ya Kimataifa ya kutokomeza Fistula ya uzazi ambapo kwa hapa nchini yatafanyika mkoani Mwanza huku yakibeba kauli mbiu isemayo ” Tokomeza fistula,Wekeza,imarisha huduma za Afya na wezesha jamii”.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa